Fursa Tano Bora za Uwekezaji Nchini Kenya

Tafsiri:
en_US

Kenya ni kitovu cha kiuchumi na usafiri ukanda wa Afrika Mashariki. Kulingana na takwimu hizi, Kenya ni taifa la kipato cha chini cha kati (wastani). Taifa hili lina idadi ya watu zaidi ya milioni 50, na takribani robo tatu ya idadi hii ya watu wana chini ya umri wa miaka 30. Licha ya nchi hii kupambana na changamoto kama vile ufisadi na msukosuko wa ukuaji wa uchumi, pana matarajio ya ukuaji mzuri. Kwa hiyo, makala haya yataangazia fursa tano bora za uwekezaji nchini Kenya.

investment kenya
Ujenzi ni mojawapo ya fursa bora ya uwekezaji nchini Kenya.

Uchumi wa Kenya ni Mkubwa kwa Kiasi Gani?

  • Mwaka wa 2018, Pato la Taifa kwa wananchi lilikuwa zaidi ya $ 1,800 ikilinganishwa na $ 1,690 kutoka mwaka 2017
  • Katika 2018, jumla ya Pato la Taifa ilikuwa kuhusu $ bilioni 87.
  • Benki ya Dunia imetambulisha kwamba, uchumi umeongezeka kwa asilima 5.7 na bado unatarajiwa kuongezeka zaidi kwa 5.9% katika mwaka 2020. Uchumi wa Kenya ni mojawapo wa chumi zinazokua kwa kasi barani Afrika.

Faida za Kuwekeza Nchini Kenya ni Zipi?

  • Uwezo wa kupata soko kubwa. Hii inatokana na lilipo taifa kijiografia na kuwa na uanachama muhimu ya chumi za kikanda pamoja na kuifanya kuwa kama lango kuu la Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA). Pia, Kenya ina mikataba mbalimbali ya kibiashara kama vile AGOA ambayo inawezesha bidhaa kufikia masoko ya mataifa yaliyoendelea kama vile Marekani bila kutozwa kodi. Kenya pia ni mwanachama wa Mkataba wa Bara Afrika wa Biashara Huru.
  • Uchumi mkubwa katika Afrika Mashariki. Licha ya changamato za msukosuko wa kiuchumi, nchi hii imekuwa imara na imeonyesha ongezeko la kasi kwa kitengo chake cha kati cha wakaazi wa mijini na hivyo kuibua mahitaji ya bidhaa za thamani ya juu. Pato la Taifa la Kenya ni zaidi ya nusu ya Afrika Mashariki nzima. Kutokana na hili, taifa hili limeishia kutambulika kwa kuwa na uchumi mkubwa katika eneo hilo.
  • Upatikanaji wa wafanyakazi wenye ujuzi. Sababu nyingine ambayo imewezesha kuwepo kwa fursa mbalimbali za uwekezaji nchini Kenya ni kuwepo kwa idadi kubwa ya wananchi wenye ujuzi na tajiriba. Wafanyakazi hawa ni zao la taasisi za kielimu nchini Kenya, Afrika, na kwingineko.
  • Amani na utulivu. Ikilinganishwa na nchi nyinginezo za Afrika ambazo zimeshuhudia vita kwa muda, Kenya ni nchi yenye amani.

Hatari za Kuwekeza nchini Kenya ni Zipi?

Kenya, sawia na mataifa mbalimbali yaliyoendelea na yanayoendelea, ina changamoto mbalimbali. Kwa hivyo, wawekezaji wanahitajika kuwa na subira na ukakamavu wakati wanapowekeza katika uchumi wa Kenya kwa sababu zifuatazo:

  • Rushwa. Katika mwongo mmoja uliopita, kumekuwa na kashfa kadhaa za matumizi mabaya ya rasilimali kwa kuwashirikisha maafisa wa umma. Fedha zinazofujwa, kwa kawaida, hulenga miradi ya maendeleo. Iwapo itakuwa vigumu baadae kutekeleza miradi hii, pana uwezekano wa kudhoofisha uchumi.
  • Migogoro ya kisiasa. Tangu machafuko ya 2007-2008 ya baada ya uchaguzi, wawekezaji na umma wameishia kupunguza shughuli yao ya kibiashara wakati wa uchaguzi wa urais. Hata hivyo, kutokana na kuhamasishwa kwa umma, hali hii inatarajiwa kuboreka katika miaka ijayo.
  • Mabadiliko ya hali ya hewa. Duniani kote pana kilio kinachotokana na mabadiliko ya hali ya hewa, na Kenya haijawachwa nyuma. Kilimo huchangia asilimia 25 ya Pato la Taifa kila mwaka na huchangia asilimia 70 ya ajira. Kwa sababu wakulima wengi hukuza mazao kwa kutegemea mvua, mabadiliko ya mwenendo wa mvua huashiria uwekezaji hatari katika kilimo.

Fursa Tano Bora za Uwekezaji nchini Kenya

Utoaji wa Huduma za Afya

big four agenda healthcare kenya
Huduma za afya ni mojawapo ya mihimili ya Ajenda Nne Kuu.

Serikali ya sasa ilianzisha Ajenda Nne Kuu kwa nia ya kuelekezea mtazamo wake katika maeneo manne ya kimaendeleo yanayokusudia kuboresha maisha ya wananchi wake. Kwa vile utoaji wa huduma za afya ni miongoni mwa nguzo hizi, imeibuka kuwa mojawapo ya fursa bora ya uwekezaji nchini Kenya. Kwa sasa inachangia asilimia 2 ya Pato la Taifa na inatarajiwa kukua kwa imara kutokana na sababu zifuatazo:

  • Idadi ya watu imepita milioni 50 na imekuwa ikikua kwa asilimia 2.5% kila mwaka.
  • Kumekuwa na ongezeko la visa vya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
  • Kuna kuongezeka kwa uelewa kuhusu dawa ya kuzuia na tiba mbadala.
  • Kuna ongezeko la matumizi ya teknolojia yanayolenga kuongeza ubora na ufanisi wa huduma za matibabu zaidi.

Fursa za uwekezaji katika sekta ya afya nchini Kenya ni pamoja na teknolojia ya matibabu, bima ya afya na maisha, pamoja na hospitali ambazo hutoa huduma za kijumla au huduma maalum za matibabu. Ili kuwekeza katika sekta hii, mtu anaweza kutumia mfumo wa uwekezaji wa kimtaji. Kwa kuwekeza katika kampuni zilizostawika au zinazochipuka ambazo zipo katika nafasi nzuri kimikakati katika vitengo vilivyotambulishwa hapo juu ni hatua yakinifu. Vilevile unaweza kuanzisha kampuni ndani ya vijisehemu tofauti katika sekta ya afya; huu utakuwa uwekezaji wa busara.

Kilimo

investment kenya
Wakulima wadogo nchini Kenya.

Usalama wa chakula pia ni mojawapo ya mihimili ya Ajenda Nne Kuu. Serikali imenuia kuisaidia sekta ya kilimo ambayo kwa sasa inachangia takriban asilimia 25 ya Pato la Taifa kila mwaka. Mbali na kuwa na mojawapo ya vyanzo vya kimsingi vinavyousogeza mbele uchumi wa nchi hiyo, kilimo kimechangia kulisha idadi ya watu inayoendelea kukua kwa kasi. Isitoshe, wakulima wengi wamekumbatia dhana ya kilimo biashara. Dhamira kuu ya wakulima ni kuwalisha wakazi, na pia kufaidika kutokana na mifumo ya serikali ya kuwezeshwa kwa biashara za kimataifa, na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Kutokana na mahitaji makubwa ya mazao ya kilimo na msaada kutoka kwa serikali, sekta hii imeishia kwa kama mojawapo ya fursa bora ya uwekezaji nchini Kenya.

Mojawapo ya njia za kuwekeza katika sekta hii ni kwa njia ya uwekezaji wa kimtaji. Baadhi ya makampuni unayoweza kutumia katika uwekezaji ni pamoja na yale ambayo yanajihusisha moja kwa moja katika kilimo cha bustani, mazao ya biashara, au mazao ya chakula. Vileile, inawezekana kuwekeza katika kampuni ambazo zinahushishwa na wakulima kwa njia nyinginezo kama vile wale ambao kuhusika katika huduma za kifedha kwa wakulima, mashine, mbolea, na usindikaji wa bidhaa. Njia nyingine ya kuwekeza katika sekta hii ni kwa kununua hisa za kampuni zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Nairobi kama vile Kakuzi Limited, Limuru Tea Plc, na Sasini.

Mali Isiyohamishika

Kama nchi yoyote ile, mojawapo wa vigezo vinavyoibua utulivu wa kifedha kwa mtu binafsi ni uwezo wa kumiliki nyumba. Jinsi tabaka la kati linavyoendelea kukua na kuelekea kiwango cha uchumi wa kati, Wakenya wengi zaidi wameweza kutimiza ndoto hii. Pia, kuna msaada wa kutosha kutoka kwa serikali ya kitaifa kwani inajitahidi kufikia azma yake ya kuwezesha kumiliki makazi ya gharama nafuu katika maeneo ya mijini na maeneo ya pembezoni.

Pia, pana ongezeko la mahitaji ya maeneo ya ujenzi kwa ajili ya biashara. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa na huduma mbalimbali, kampuni na watu binafsi katika sekta hii wameuchangamkia ununuzi wa ardhi kwa ajili ya miradi ya maendeleo au kwa kutarajia kuongezeka kwa thamani ya ardhi. Kwa hakika, hii ni mojawapo ya njia zenye faida ya kuwekeza katika sekta hii. Isitoshe, unaweza kujihusisha na mali isiyohamishika nchini Kenya kupitia uwekezaji wa kimtaji au kwa kununua hisa za kampuni husika.

Uzalishaji wa Kiviwanda

Kenya inajitahidi kuwa nchi ya viwanda kwa kujumuisha sekta hii katika mihimili ya Ajenda Nne Kuu. Serikali imeendelea kutoa mazingira mazuri kwa wazalishaji ili kukidhi kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa nchini na hata masoko ya kimataifa. Kuwepo kwa wafanyakazi wenye ujuzi kwa gharama nafuu na kuwepo kwa malighafi nafuu kumeifanya sekta ya viwanda kuwa fursa bora ya uwekezaji nchini Kenya. Baadhi ya sekta ndogo ambazo wazalishaji wanaweza kuwekeza ni pamoja na nguo, kilimo, plastiki, dawa, chuma, na viwanda vya kemikali.

Mtu anaweza kuwekeza sekta hii kupitia uwekezaji wa kimtaji katika moja au zaidi ya kampuni imara na hata zile zinazokua. Pamoja na haya, unaweza kununua hisa za kampuni zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Nairobi kama vile Bamburi Cement, Crown Paints, na Unga Limited. Mbinu nyingineyo ya kuwekeza katika sekta hii ni kwa kuanzisha kampuni ambayo inasambaza malighafi au kutoa huduma za uchukuji zinazohitajika na wazalishaji wa viwanda.

Ujenzi

investment opportunities kenya
Maendeleo ya miundomsingi kama vile mabwawa ni njia bora ya uwekezaji nchini Kenya.

Kenya ni mojawapo wa nchi zinazoendelea barani. Kwa hivyo, kuna miradi mbalimbali ya ujenzi inayoendeshwa. Serikali pamoja na kampuni binafsi zimejishirikisha katika shughuli za ujenzi kama vile kujenga mabwawa, njia ya usafiri (barabara na reli), shule, hospitali, na pia majengo ya makazi na biashara. Hali hii inaufanya ujenzi kuwa mojawapo ya fursa bora ya uwekezaji nchini Kenya. Kuwepo kwa wafanyikazi wenye ujuzi kwa gharama nafuu pia kumechangia katika ukuaji na kuendelea kwa sekta hii.

Ununuzi wa hisa za kampuni kama vile Bamburi Cement na East Africa Portland Cement ni moja ya njia ambazo unaweza kutumia ili kuwekeza katika sekta hii. Vilevile, mwekezaji anaweza kuwekeza mtaji kwa kutambua kampuni zilizostawika au hata zinaochipuka na zinazodhihirisha uwezo mkubwa. Pia, ni faida ukianzisha kampuni inayosambaza vifaa vya ujenzi kwa watu binafsi, makampuni, na serikali. Kadhalika, unaweza kuanzisha kampuni ambayo inalenga tu kupata zabuni ya kukamilisha miradi maalum ya ujenzi.

Hitimisho

Kenya ni mojawapo wa nchi za ulimwengu wa tatu barani Afrika. Licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali na kuwa kizingiti kwa wawekezaji, kuna fursa za faida za uwekezaji. Kwa kujitia katika nafasi ya kimkakati katika sekta hizi, mwekezaji ana nafasi ya kipekee ya kupata bonge la faida.