Makosa Ya Pesa Ya Kuepuka

Tafsiri:
amen_US

Watu hukumbwa na shida za kifedha wakati fulani katika maisha yao. Baadhi ya shida hizi za kifedha husababishwa na makosa kadhaa ya pesa. Katika makala haya, tutaangazia makosa kadhaa ya pesa ambayo unapaswa kukwepa ili uweze kuwa huru kifedha.

Makosa Ya Kifedha Ya Kuepuka Ukiwa Miaka 20

1. Kukosa kupanga

Hatua ya kwanza ya kujipatia uhuru wa kifedha ni kuwa na mpango wa matumizi, ama makadirio ya bajeti. Ziwekee mpango pesa zako kabla ya kulipwa. Hakikisha kuwajibikia kila senti unayopata na hakikisha unaitumia kwa njia mwafaka. Mpangiio kama huu utakusaidia kuzuia gharama za kighafla ambazo mara nyingi hutokea kila siku na kuishia kuongezeka kwa muda mrefu na hatimaye kuwa kiwango kikubwa. Kuandaa bajeti pia kutahakikisha kuwa unaweka kando akiba ambayo inaweza kukusaidia wakati wa dharura.

Ili kuwa na mpango mzuri wa fedha, unaweza kutumia programu za udhibiti wa fedha kama vile Mipango App na Money Lover.

2. Kutoweka Akiba

Katika miaka yako ya 20, huu huwa umri unaofaa na unastahili kuanza kuweka akiba kwa sababu za dharura na kustaafu kwako. Njia bora ya kutimiza malengo kama haya ni kuwa na makadirio ya bajeti; unafaa kuyaandika mahitaji yako ya kifedha na utilie maanani mpangilio huo. Pindi unapolipwa, kwanza tenga akiba na unaweza kutumia masalio. Unahitaji kutenga angalau asilimia 15 ya mapato kama akiba.

3. Kununua Gari Mapema

Sio wazo zuri kununua gari ukiwa miaka 20 hivi. Katika umri huu, unapaswa kuwa unajiwekea msingi mzuri wa maisha yako ya baadaye. Gari lina gharama na utahitajika kulipia bima na pia ada nyinginezo zinazohusisha kulidumisha gari hilo. Pesa hizo ungezitenga kama akiba au kuzielekeza katika miradi ya kuzalisha mapato ya kiziada. Pia, kuna gharama ya uchakavu wakati utahitaji kuliuza hilo gari. Badala ya kununua gari, wekeza pesa hizi katika mradi ambao utakuwa unazalisha pesa zaidi.

4. Kuishi Zaidi Ya Uwezo Wako

Watu wengi katika miaka yao ya 20 huwa wanaishi zaidi ya uwezo wao (wa kifedha)na kuishia kuwa na madeni. Unapaswa kutumia pesa kidogo kuliko mapato yako ili ubaki na akiba kiasi. Tatizo kubwa ni kwamba vijana wengi wanataka kujilinganisha na wenzao. Hakuna faida ya kununua vitu ambavyo huwezi kuvimudu, kwani vitakuongezea tu madeni. Kutokana na mtazamo huu, usinunue gari ikiwa huna uwezo wa kulipa. Hata hivyo, ikiwa ni lazima ujipatir gari, itakubidi ujiwekee akiba ya kulinunua ila usinunue kwa njia ya deni.

Makosa Ya Kifedha Ya Kuepuka Ukiwa Miaka 30

1. Kulipa Madeni Kwa Kutumia Akiba Yako

Ukihitimu miaka 30, watu wengi kwa kawaida huwa wameweka akiba. Hata hivyo, watu wengi hufanya makosa ya kuyalipa madeni yao kwa kutumia pesa walizohifadhi kama akiba. Njia bora ya kulipa deni lako ni kutokana kwa miradi inayozalisha mapato. Pia, inakupasa kujizuia kujiingiza kwenye deni lisilo la lazima. Hii itakusaidia kutotumia akiba yako kulipa deni kama hilo. Pia, kabla ya kupata mkopo, ni bora kuwa na mpangilio wa jinsi ya kulipa deni hilo.

2. Kugharamikia Sana Nyumba Yako

Ni bora ujenge au ununue nyumba ambayo inatosheleza mahitaji yako. Hapana haja ya kujenga nyumba kubwa zaidi ya unavyohitaji. Nyumba yako sio mojawapo wa mfumo wa uwekezaji kwa vile haikuzalishii pesa; na hivyo basi huhitajiki kughamarika sana kwa ajili ya nyumba. Badala yake, elekeza fedha hizo kwa mradi unaozalisha mapato. Ikiwa nyumba yako ni kubwa sana, unaweza kuikodisha na wewe ukodishe nyumba ndogo inayofaa mahitaji yako.

3. Kuutegemea Mshahara tu

Unahitaji kuwa tayari ikiwa kutatokea kusambaratika kwa uchumi au nyakati za dharura. Pia, unahitajika kuwa na mpango wa ikiwa utapoteza kazi yako. Kutokana na hili, ukitimia miaka 30, unapaswa kuanza kuwekeza na kujiandaa kwa ajili ya kustaafu kwako. Hivyo basi, ili kuepuka kuishi kwa kuutegemea mshahara wako tu, unahitaji kuwa na makadirio ya bajeti na pia kuishi ndani ya mipaka yako ya kifedha.

4. Kukosa kuwekeza

Ni bora unapoanza kuwekeza mapema. Unapoanza kuwekeza ukiwa na miaka 30, uwekezaji wako utaanza kukuzalishia mapato mapema na utakuwa na vyanzo vingi vya mapato badala ya kuitegemea kazi yako ya kawaida. Hii inakuandaa unapolenga kustaafu, ili hata unapoacha kufanya kazi, bado utakuwa na vyanzo vya kukuletea mapato. Kwa mfano, unaweza kuwekeza katika biashara za mali isiyohamishika ambayo inaweza kukupa mapato mwishoni mwa kila mwezi.

Makosa Ya Kifedha Ya Kuepuka katika Biashara

Ikiwa unamiliki biashara, unahitaji kuwa na ufahamu wa makosa yafuatayo ya kifedha na jinsi ya kuyaepuka.

1. Kukosa kuwa na Makadirio ya Bajeti

Ili kusawazisha kati ya mapato na gharama yako ya biashara unahitajika kuwa na bajeti. Unahitaji pia kujua wakati upi wa kupunguza matumizi/gharama zako ili kuzuia hasara. Kwa mfano, ikiwa utagundua kuwa kutakuwa na kupungua kwa mauzo, unaweza kujitafutia njia za kupunguza gharama za biashara yako.

2. Kuchanganya Fedha Za Biashara na Fedha Za Kibinafsi

Unahitaji kutenganisha pesa zako binafsi na zile za biashara yako. Ni bora kufungua akaunti ya biashara. Kuwa na akaunti tofauti na biashara yako itakusaidia kuweka rekodi ya mapato ya biashara. Pia itakusaidia kujua ikiwa biashara inazalisha faida yoyote. Ikiwa utaongeza pesa za kibinafsi kwenye biashara, unaweza kuichanganya na kuona kama faida.

3. Kuweka Bei ya Chini Sana

Wakati ushindani uko juu, biashara nyingi hulazimika kushusha bei ya bidhaa na huduma zao. Hii huwa mazoea ya kawaida kwa biashara ndogo ambazo zinaanza tu. Unastahili kuangazia hesabu za gharama zote za biashara wakati wa kuweka bei ya bidhaa na huduma. Bei za chini zinaweza kufanyika suluhu japo kwa muda mfupi, Kwani itakufanya ufunge biashara yako. Walakini, unahitaji pia kuwa mwangalifu wakati wa kuweka bei ili kuzuia kuzidisha bei ikilinganishwa na washindani wako.

4. Kuzidisha Gharama ya Uzinduzi wa Biashara

Mara nyingi, watu wengi wanapoanza biashara huwa na matumaini ya juu sana ya jinsi biashara zao zitakua. Ni jambo zuri lakini ni muhimu pia kuwa na mtarajio halisia. Ni bora uanze kwa kiwango kidogo na baadaye kupanua biashara yako kulingana na mahitaji ya bidhaa na huduma. Kwa kutumia mfumo huu, itakuzuia kutumia gharama kubwa ya kuanzisha biashara yako. Hivyo basi, utahitajika kuwa na bajeti ya kuanzisha biashara na uitilie maanani. Mara tu biashara yako inaponawiri na kuendelea, unaweza kuipanua wakati tu inahitajika.

5. Kukosa Kujilipa

Watu wengi hukosa kufidia juhudi ambazo wamechangia katika biashara na hivyo kuishia kutojilipa wenyewe. Unahitaji kugundua kuwa wewe ni mwajiri wako mwenyewe na kwa hili unahitaji kulipwa. Kwa hivyo, unahitaji kujumuisha mshahara wako katika gharama za biashara yako. Hii itakusaidia kutekeleza gharama za kibinafsi bila kuzitumia pesa za biashara. Usijilipe kiwango cha chini cha inavyostahili. Kwa hali yoyote ile, jilipe ​​mwenyewe kama vile ungemlipa mfanyakazi wako akitoa huduma kama hizo.

6. Ukosefu Wa Mtaji Wa Kutosha Wa Kufanya Kazi

Ukosefu wa mtaji wa kufanya kazi ni shida ya kawaida kwa biashara ndogo ndogo. Unapoanzisha biashara, ni bora kuwa na mtaji wa kutosha wa kufanya kazi ambao unaweza kukimu mahitaji yako ya kibiashara kwa angalau miezi 6. Mtaji huu utakuzuia kukopa ili kudumisha gharama za biashara yako. Haimaanishi kuwa si sawa kutafuta mikopo ya kibiashara. Muhimu ni kutambua kuwa kwa kawaida mikopo hii huwa na kiwango fulani cha hatari.

Hitimisho Kuhusu Makosa Ya Kifedha Ya Kuepuka

Ili kupata uhuru wa kifedha, unahitaji kuyazuia makosa haya ya kifedha tuliyoya tambulisha. Njia bora ya kuyatekeleza ni kwa kujiwekea bajeti kwa gharama zako na akiba. Mara tu ukiwa na bajeti, unahitaji kuifuatilia na hivyo kukuepusha kutokana na gharama zinazoweza kuzuilika. Gharama hizo ambazo hazijazuiliwa zinaweza kuonekana kuwa ndogo lakini huishia kuongezeka na kuwa gharama kubwa.