Ulaghai wa Biashara za Kubadilisha Fedha za Kigeni

Tafsiri:
No available translations found

Ubadilishaji wa fedha za kigeni ni mchakato wa kubadilisha fedha moja kwa nyingine. Kubadili pesa za Kigeni kwa mtandao kumepata umaarufu barani Afrika ambapo wawekezaji watarajiwa wanaahidiwa mapato makubwa na ya haraka, hivyo basi kuongeza ulaghai huu katika bara pia. Unawezaje kujilinda dhidi ya ulaghai huu?

Mambo ya Kuvutia

» Baadhi ya sababu za kuongezeka kwa biashara za ubadilishaji wa fedha za kigeni ni ukosefu wa ajira, kupanda kwa gharama za maisha na kupenya zaidi kwa intaneti. Biashara hii, kwa kiasi kikubwa inafanywa na vijana wa Afrika, walioelimika, na wenye ufahamu wa teknolojia kama chanzo mbadala cha mapato.

» Inakadiriwa kuwa karibu Naira milioni 350-450 hufanyiwa biashara kila siku nchini Nigeria na idadi ya wafanyabiashara rejareja wa ubadilishaji wa fedha za kigeni nchini humo inaweza kuwa kama 300,000. Kwa wastani, wafanyabiashara wa ubadilishaji wa fedha za kigeni Afrika Kusini hufanya amana ya karibu $742 baada ya miezi mitatu.

Chati kama hizi zinaweza kughushiwa.
Chati kama hizi zinaweza kughushiwa.

Ulaghai wa Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni

Kiasi cha ulaghai wa ubadilishaji wa fedha za kigeni ni cha juu na gharama za ulaghai huweza kuwa za juu sana. Kwa mfano, wawekezaji 13,000 nchini Kenya walipoteza zaidi ya bilioni Sh1.1 kwa kampuni ya VIP Portal mwaka wa 2015. Hadi sasa, hii bado inachukuliwa kuwa kashfa kubwa ya ubadilishaji wa fedha za kigeni katika historia ya Kenya.

Hivi karibuni, Jabulani ‘Mr Cashflow’ Ngcob, wa Afrika Kusini alihukumiwa miaka 6 jela mwezi Mei, 2019. Ngcobo (33) alidai kuwa milionea akiwa mtendaji mkuu wa Cashflow Pro, kampuni ya ubadilishaji wa fedha za kigeni. Alichapisha kitabu mwaka wa 2018 “Cashflow Naked” kuhusu maisha yake na jinsi alifanikiwa katika biashara ya ubadilishaji wa fedha za kigeni na pia kutoa vidokezo vya kifedha kwa jamii za kipato cha chini.

Ushuhuda wa kibinafsi unaweza vilevile kuhuzunisha sana. Mkaazi mmoja wa Afrika Kusini alipoteza R100,000 Mei mwaka huu baada ya kupata habari kwenye YouTube yenye madai kuwa Waafrika Kusini wanapata fedha katika biashara ya ubadilishaji wa fedha za kigeni. Alifuata kiungo na kuishia kwenye tovuti ya KontoFX (kampuni yenye kashfa ya ubadilishaji wa fedha za kigeni) na kufungua akaunti kwenye tovuti. Hata hivyo, baada ya kupata fedha kwenye tovuti, hakuweza kuzitoa fedha zake.

Mwaka wa 2018, Waafrika Kusini zaidi walipoteza fedha kutokana na ulaghai wa biashara za ubadilishaji wa fedha za kigeni zilizoendeshwa kwa zaidi ya miaka miwili kutoka Ufilipino.

Nchi nyingine kama vile Nigeria zimeathirika pia. Mwaka 2015, kampuni ya ubadilishaji wa fedha za kigeni inayoitwa BTD Multi-Global Company iliwaahidi Wanigeria kuwa wangepata faida ya 20% kila mwezi. Kufikia 2017, wawekezaji hawakuweza tena kuziondoa fedha zao. Inaaminika kuwa, karibu watu 3,500 walilaghaiwa jumla ya Naira bilioni mbili za Nigeria.

Mwezi Aprili 2019, Benki Kuu ya Zambia, Tume ya Kumpambana na Madawa ya Kulevya na Kituo cha Ujasusi wa Kifedha walitangaza kuichunguza kampuni ya kifedha inayoshiriki katika biashara ya fedha za kigeni iitwayo “Microsavers Hub”. Mamlaka ilisema kuwa kampuni ilikuwa imeshiriki katika operesheni ya uwekezaji ambayo hulipa faida kwa wawekezaji wake kutoka fedha zao au fedha zilizolipwa na wawekezaji wapya.

Mitandao ya kijamii kama Facebook huwa mojawapo wa sehemu zinazotumika kama maeneo ya kuendesha biashara hizi tapeli.

Jinsi ya Kujilinda Dhidi Ulaghai wa Biashara ya Kubadilisha Pesa za Kigeni

Kama una nia ya kujihusisha na biashara ya ubadilishaji wa fedha za kigeni, hakikisha kuwa unapata elimu ya kutosha kuhusu jinsi ya kuendesha biashara za ubadilishaji wa fedha za kigeni kabla ya kuwekeza. Ubadilishaji wa fedha ni biashara ngumu sana, tata na huhitaji muda mwingi. Fahamu kwamba kutarazaki kutoka ubadilishaji wa fedha ni vigumu sana au haiwezekani kamwe.

Utafiti unaonyesha kwamba haiwezekani kwa mtu binafsi kujikimu kwa aina hii ya biashara. “Tumeona kuwa watu wote ambao walianza biashara hii kati ya 2013 na 2015 katika soko la hisa la Brazil na wakadumisha angalau kwa siku 300: asilimia 97 yao walipoteza fedha, asilimia 0.4 wakapata pesa zaidi kuliko wahudumu wa benki (US $ 54 kwa siku) na wale wa juu zaidi walipata US $ 310 kwa siku”

Fanya Utafiti Kuhusu Madalali wa Ubadilishaji wa Fedha za Kigeni

Mbali na kuelewa maswala muhimu, unahitaji pia kufanya utafiti kuhusu dalali unayetaka kufanya biashara naye. Kwa mfano, jihadhari na madalali ambao wanaahadi mapato yatakayokufanya milionea katika kipindi cha muda mfupi. Jiulize kwa nini mtu mgeni, usiyemjua uliyekutana tu naye kwenye mitandao ya kijamii, anataka kukufanya milionea.

Lazima pia uwe na wasiwasi kama hakuna taarifa za kutosha kwenye tovuti ya biashara ya kampuni ya ubadilishaji wa fedha kama vile ikiwa kampuni hiyo inadhibitiwa, imekuwa katika biashara kwa muda gani, anwani, majina ya watu halisi, nk

Baadhi wadanganyifu wa ubadilishaji wa fedha hutumia taarifa za biashara bandia, picha za viwambo au akaunti za maonyesho tu ili kuvutia wawekezaji wasiofahamu. Tahadhari wakati wa kushughulika na wafanyabiashara ambao wanatumia mbinu zenye hima, shuhuda zinazovutia kupitiliza na kujionyesha kuhusu “utajiri wao”.

Ushuhuda kama huu mara nyingi ni utapeli.

Ishara za Udanganyifu wa Ubadilishaji wa Fedha za Kigeni

Ishara nyingine za kukupa wasiwasi na kuonyesha unaweza kuwa unashughulika na wadanganyifu ni wakati huwezi kutoa fedha zako na mfanyabiashara huyo anasisitiza kuongeza fedha zaidi katika akaunti yako, wafanyabiashara ambao wanadai kumiliki mfumo utakaokuzalishia kiasi kikubwa cha fedha wakati wewe unalala na wafanyabiashara ambao kuweka fedha zako katika mchango wa ubia ambapo huwezi kufuatilia uwekezaji wako wa kibinafsi.

Mtaalamu wa fedha wa Afrika Kusini, Craig Gradidge, anasema tuifikirie biashara ya ubadilishaji wa fedha za kigeni kama mbadala wa kucheza kamari. Kwa hiyo, unapaswa kushiriki katika biashara hii iwapo tu huna matatizo yoyote ya kifedha.

Biashara ya ubadilishaji wa fedha za kigeni si tofauti na kamari…kama wewe si mfanyabiashara shupavu au huna ujuzi na uzoefu ipasavyo, ni lazima kuepukwa kabisa […], anasema Craig Gradidge.

Hitimisho

Ubadilishaji wa fedha ni biashara halali. Hata hivyo, kuna kampuni nyingi zenye udanganyifu na huwavutia Waafrika kwenye intaneti na mitandao ya kijamii. Si uwekezaji wa kupata utajiri wa haraka. Ili kupata faida nzuri, unahitaji mafunzo sahihi na kuhakikisha kuwekeza tu kiwango ambacho unaweza kumudu kupoteza.