Matumizi ya Teknolojia na Mipangilio ya Uraia Ili Kuondoa Ufisadi Nchini Kenya

Tafsiri:
No available translations found

Kutokana na uporaji mkubwa wa fedha za umma nchini Kenya, mashirika tofauti ya kiserikali, yasiyo ya kiserikali na raia wenyewe wameanzisha mipango mbalimbali ya kupambana na ufisadi. Maendeleo katika uvumbuzi wa teknolojia unasaidia kuondoa ufisadi.

Teknolojia inatumiwa kama moja ya masharti ya demokrasia na kujenga uwazi na kuendeleza ushiriki wa raia. Licha ya hayo, inatumika kufanya kazi za wizara za serikali kuwa wazi. Teknolojia imesaidia pia kuleta mapinduzi ya njia tofauti za ugunduzi, ukingaji na uchambuzi wa rushwa.

Anti-corruption sign in the capital Nairobi. Photo credit: Christine und Hagen Graf.
Ujumbe dhidi ya ufisadi jijini Nairobi. Picha na Christine und Hagen Graf.

Jinsi Teknolojia Inatumika Kuondoa Ufisadi

Kuna njia tofauti ambazo teknolojia inatumika ili kumaliza ufisadi. Njia zinazotumika ni zifuatazo.

1. Data Kubwa

Teknolojia inaunda uwazi na kuboresha usahihi katika michakato yote ya serikali. Teknolojia hufanya data ipatikane na inaboresha ubora wake unaosababisha maamuzi bora na uwajibikaji bora.

Matumizi ya data kubwa, mitandao iliyoboreshwa na miundombinu ya data inaweza kuhakikisha uwajibikaji bora wa matumizi ya fedha za serikali. Data kubwa pia husaidia kugundua mianya ambayo fedha za umma huporwa. Data kubwa hutumiwa katika sekta muhimu kama vile afya ya umma, biashara na utozaji wa ushuru kuamua mwenendo, mifumo na uhusiano ambapo usindikaji wa data kubwa unahitajika.

Kupitia uchangishaji wa umati, shirika la African Maths Initiative (AMI), shirika lisilo la kiserikali nchini Kenya, limeandaa programu ya R-Instat, ambayo inaweza kutumika kuchambua data ya manunuzi na kubaini viashiria vya hatari ya rushwa.

2. Ukusanyaji wa Mapato

Mamlaka ya Ushuru nchini Kenya (KRA) imekuwa na lawama kwa mianya yake mingi ambayo husababisha upotezaji mkubwa wa ushuru. Hii inatokana na ushiriiano kati ya maafisa wa KRA na wananchi ambapo wanawapa maafisa wa KRA rushwa ili kuepuka ushuru. Matumizi ya teknolojia kwa ukusanyaji wa ushuru utasaidia katika kuhakikisha kuwa ushuru uliyokusanywa unafika serikali kuu. Matumizi ya vitabu na rekodi katika ukusanyaji wa ushuru inapaswa kubadilishwa na utumiaji wa kompyuta ili ripoti ipatikane na mamlaka husika. Matumizi ya teknolojia kwa ukusanyaji wa ushuru utasaidia katika kuhakikisha kuwa ushuru uliyokusanywa unafika serikali kuu. Matumizi ya vitabu na rekodi katika ukusanyaji wa ushuru inapaswa kubadilishwa na utumiaji wa kompyuta ili ripoti ipatikane na mamlaka husika.

Utafiti uliofanywa katika kaunti ya Kiambu ulionesha kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutokana na matumizi ya kompyuta. Kulikuwa na ongezeko la asilmia 60 la ukusanyaji wa mapato.

3. Matumizi ya Teknolojia ya Kiwango cha Juu Katika Kukagua Taasisi za Serikali

Mara nyingi, ufisadi hufanyika kwasababu ya njama kati ya viongozi katika taasisi za Serikali. Hii inafanya kuwa vigumu kugundua udanganyifu mdogo. Ili kugundua udanganyifu kama huo, ni muhimu kukuza mifumo ya kiwango cha juu cha udhibiti wa ndani ili kuwazuia wahusika. Wakati wa kukagua taasisi za serikali, ni muhimu kutumia vifaa vya ukaguzi wa mahesabu vya hali ya juu ambavyo vinaweza kugundua ufisadi. Mbali na kukagua taasisi za serikali, kuweka hatua za kuzuia ufisadi kama vile kuondolewa kwa shughuli za fedha taslimu itahakikisha kuwa fedha inatumika kwa njia iliyokusudiwa.

4. Ukaguzi wa Maisha ya Maafisa Wote wa Serikali

Serikali ya Kenya ilizindua mpango wa kukagua mtindo wa maisha kwa wafanyakazi wote wa umma mnamo 2018. Serikali inazingatia utumiaji wa wafanyakazi wa umma na chanzo cha utajiri wao ili kubaini ikiwa matumizi yao yanaendana na mapato. Hii ni harakati nzuri lakini imekosolewa sana na wahusika wa ufisadi na kufanya utekelezaji wake kuwa mgumu.

Ni muhimu pia kuwa watumishi wote wa umma watangaze utajiri wao na serikali kudhibiti ikiwa takwimu ni sawa na mapato yao. Ikiwa hatua hii itatekelezwa kama Rais alivyoahidi, mali ambayo haiwezi kudhibitishwa itachukuliwa na serikali.

Transparency International Kenya (TI-Kenya) is the leading anti-corruption NGO.
Tovuti ya Transparency International Kenya (TI-Kenya), shirika lisilo la kiserikali linaloongoza mapambano dhidi ya ufisadi Kenya.

5. Mtandao na Programu Tumizi za Rununu

Programu tumizi za rununu zinatumika katika sehemu nyingi ulimwenguni kukusanya data za utawala. Kwa mfano, Benki ya Dunia ilitengeneza programu ya ‘Integrity App’ ambapo raia wa nchi zingine wanaweza kuona miradi ambayo benki hii imefadhili. Kama kuna shughuli zenye kasoro au tuhuma, zinaweza kupatikana kwa urahisi.

Action for Transparency (A4T) ni mradi wa mwasisi unaopambana kuondoa ufisadi na utumiaji mbaya wa fedha za serikali nchini Kenya kwa kuweka nguvu ya mabadiliko mikononi mwa raia. Kutumia simu ya rununu na mtandao, mtu yeyote anaweza kuangalia kiwango cha pesa za serikali iliyoahidi kwa kila shule na kliniki ya afya – na kiasi kinachotumika. Ikiwa hauna rununu isiyoweza kuingia mtandaoni, unaweza kutumia tovuti. Mtu anaweza pia kuripoti ufisadi kupitia majukwaa ya A4T.

Teknolojia nyingine ni Rada ambayo ilizinduliwa na Transparency International Kenya mnamo Juni, 2019. Teknolojia hii ni hifadhidata ambayo inafuatilia na kurekodi kesi zote za ufisadi zilizo mahakamani.
Ripoti ya Hali ya Utawala wa Kaunti ni ubao wa uchambuzi wa kina kwa kaunti zote 47 za Kenya mwaka wa 2016.

Uwajibikaji Pamoja ni mfumo wa rufaa wa malalamiko ambapo malalamiko yanawekwa na umma kutoka kaunti tano za Kenya (Marsabit, Wajir, Pokot Magharibi, Turkana, Mandera) kuhusu huduma zinazotolewa na washirika, wadau na serikali za kaunti katika kaunti hizo. Mfumo huo una uwezo wa kutuma ujumbe mwingi wa maneo kwa watu kadhaa wakati kunahitajika kusambazwa kwa wingi nyingi ujumbe wa onyo kwa idadi kubwa ya watu katika kaunti zilizotajwa hapo juu.

Orodha ya Ahadi ya Kupambana na Rushwa ya Kenya inafuatilia maendeleo ya ahadi zilitolewa na Serikali ya Kenya katika mkutano mwaka wa 2016 wa kupambana na ufisadi.

Ukaguzi wa Hesabu wa Umma ni jukwaa ambalo lina uchambuzi wa kina wa ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Serikali tangu 2013.

6. Mfumo wa Usimamizi wa Miradi ya Kaunti

Mfumo wa Usimamizi wa Miradi ya kaunti umetekelezwa katika Kaunti ya Makueni ambapo imekuwa na mafanikio. Serikali ya Kaunti ya Makueni inayoongozwa na Profesa Kivutha Kibwana ilitekeleza mfumo huo kuhakikisha uangalizi, uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma. Kupitia mfumo huo, umma unaweza kuona jinsi fedha zinatumika katika miradi.

Kaunti ya Makueni imeorodheshwa kuwa kaunti bora zaidi nchini Kenya katika usimamizi wa fedha na yenye rekodi bora ya maendeleo. Kutekelea mfumo huu katika kaunti zingine, Kenya itakuwa imepiga hatua mkubwa katika kupigana na ufisadi.

Hitimisho

Kupigana na ufisadi nchini Kenya ni jambo la lazima. Kwa hivyo, mipango zaidi ya kiteknolojia kutoka ndani na nje ya Kenya inapaswa kutekelezwa. Kenya inafanya maendeleo katika kupigana na ufisadi kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai. Ofisi hizo mbili hadi sasa zimefanya uchunguzi na kushtaki watu kadhaa wanaohusishwa na ufisadi. Kwa mkazo kuwa ufisadi unaweza kumalizika.

Soma Zaidi