Biashara ya Teknolojia za 3D

3D Africa ni mradi wa kielimu na mafunzo ambao unafundisha uchapishaji kwa teknolojia ya 3D (uchapishaji wa pande tatu), jinsi ya kuuza vitu tofauti unavyoandaa na jinsi ya kujijengea biashara au kazi kupitia uchapishaji wa 3D.

3D Africa ni mradi uliozinduliwa na Youth for Technology Foundation, waandalizi wa programu za elimu, mafunzo, na za uwezeshaji wa kiuchumi barani Afrika na nchi nyingine zinazoendelea.

3D printing in Africa

Shirika hili hufanikisha haya kwa usaidizi wa wakufunzi wa darasani na mtandaoni. Washiriki hujifunza jinsi ya kupanga, kubuni, na kutengeneza bidhaa zilizochapishwa kwa njia ya 3D ili kuweza kuuza hadi mtandaoni. Programu hii inahusisha ujuzi wa kiufundi, elimu, mafunzo ya kibiashara, na usaidizi hata baada ya mafunzo; ili washiriki waweze kuajiriwa katika sekta zinazojihusisha na sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati, kuanzisha biashara, kuzindua vyanzo vipya vya mapato, au hata kupata kazi nzuri na kukuza taaluma.

Maelezo ya Haraka Kuhusu Uwezo wa uchapishaji wa 3D

  • Iwapo mtoto alizaliwa bila mkono—unaweza kutumia teknolojia ya 3D kumtengenezea mtoto huyo mkono.
  • Mafuriko yanaposababisha hasara kwa nyumba—unaweza kutumia teknolojia ya 3D kuijengea tena jamii yako nyumba.
  • Ikiwa watoto kijijini mwako hawana vifaa vya kuchezea, teknolojia hii ya 3D inaweza kusaidia kutayarisha vifaa hivyo bandia vya kuchezea.

Je, Uchapishaji wa Teknolojia ya 3D ni Nini Hasa?

Uchapishaji wa 3D ni utaratibu wa kujenga vitu vya pande tatu kwa usaidizi wa kompyuta inayofuata mfano au kielelezo, na kwa kawaida hufanyika kwa mfululizo wa kuongeza nyenzo, safu kwa safu, inayopelekea kujulikana kama uzalishaji viwandani wa nyongeza.

Mustakabali wa Uchapishaji wa Kidijitali Barani Afrika

Afrika imeonyesha uwezo wa ajabu wa kuasi aina ya zamani ya teknolojia na badala yake kukumbatia teknolojia ya kisasa. Bara hili lilikwepa matumizi ya simu za jadi za mezani na za nyaya, na kuhamia moja kwa moja kwa simu za mkononi na mawanda tamba mapana (wireless broadband).

Kwa mujibu wa 3D Africa, uzalishaji wa kidijitali wa viwandani na uchapishaji kwa mfumo wa 3D utaibua mageuzi katika sekta za viwanda barani Afrika jinsi simu tamba za kisasa zilivyoleta mageuzi ya huduma, biashara, na viwanda vya kilimo. Ukosefu wa sekta imara ya viwanda unamaanisha kuwa, Waafrika wengi wanategemea kuagiza bidhaa kama vile sehemu za mashine, bidhaa za matumizi, bidhaa za nyumbani, zana, na vifaa vya ujenzi. Teknolojia hii ya uchapishaji ya 3D ina uwezo wa kupunguza utegemezi wa bidhaa ghali zinazotoka nje.

Kubadilisha Bara kutoka ‘Msaada kwa Afrika’ hadi ‘Imetengenezwa barani Afrika’ – Njideka Harry, Rais na Mkurugenzi Mtendaji, Youth for Technology

Faida Zinazotokana na 3D Afrika kwa Washiriki

  • Kujiandaa kwa ajili ya nafasi mpya ya kazi.
  • Kuwa na mapato saa ishirini na nne kwa wiki (24/7) ukiwa nyumbani, katika vitovu vya kidijitali, au mahali pa biashara.
  • Kuanzisha biashara za ujasiriamali.
  • Kuvumbua bidhaa mpya.
  • Kuwapata wateja wapya.
  • Kupenyeza katika masoko mapya.
  • Kushiriki katika mifumo ya kibiashara ya kimataifa mtandaoni.
  • Kuzalisha bidhaa dukani moja kwa moja badala ya kununua kutoka wauzaji wa kijumla, wauzaji wa rejareja, au kwa kuagiza.

Jinsi Programu Hii Hufanya Kazi

3D printing africa
Mashine ya uchapishaji ya 3D.

3D Africa huwapa washiriki matini ya kusoma, mafunzo ya kiutendaji, na usaidizi wa kitaalamu wakati na baada ya kuhitimu, ili kuwawezesha kubuni, kuzalisha, na kuuza baadhi ya bidhaa zilizochapishwa kwa njia ya 3D. Washiriki hujumuisha wanafunzi, wale wanaotafuta ajira, wamiliki wa biashara, au wajasiriamali wanaonuia kuanzisha biashara barani Afrika.

Ili kujiunga na mpango huu, unahitaji kujiandikisha kwa kujaza na kukamilisha fomu mtandaoni. Mmoja wa wanachama wa timu ya 3D Africa atawasiliana nawe kukueleza hatua zaidi kuhusu maombi yao pindi tu wanapopokea habari zako.

Jinsi Madarasa Yanavyoandaliwa

3D printing in africa
Washiriki wa 3D Africa.

Madarasa yamepangwa kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari, wanafunzi wa vyuo vikuu, wanaotafuta ajira, na vileveile kwa ajili ya wanawake na wajasiriamali vijana. Mafunzo yote hutumia mchanganyiko wa mtaala wa mtandaoni (MOOCs) na mafunzo ya ana kwa ana kupitia kwa wakufunzi wa 3D Africa.

Vikundi vyote hujifunza masuala ya kiufundi na kibiashara yanayohusu uchapishaji wa 3D na hurejelea:

  • Kujifunza kutumia programu, vifaa, na programu za vielelezo.
  • Kufanya kazi katika mazingira ya maabara kama sehemu ya timu inayoshughulikia kupanga, kuvumbua, kuonyesha, na pia kufanya marekebisho kwa vielelezo vya uchapishaji vya 3D ili viweze kuafiki na kusuluhisha matatizo halisi ya dunia.
  • Kukutana na washauri ili kuweza kuzindua fursa za ujasiriamali mtandaoni kwa bidhaa za 3D zilizochapishwa.
  • Kufanya kazi katika maeneo teule ya kujifunzia pale ambapo wanafunzi wanapata kuifanya kazi miradi yao binafsi au kuanzisha biashara ya ujasiriamali.

Wanafunzi wa vyuo vikuu wanaweza kutuma maombi kuwa mabalozi wa teknolojia wa 3D Africa katika vyuo vikuu yao. Wanaotafuta kazi hujifunza ujuzi mbalimbali unaohusiana na 3D unaotafutwa na waajiri. Aidha, wao pia hujifunza kuhusu maswali yanayofungamanishwa na bidhaa za 3D ikiwemo mauzo, huduma kwa wateja, ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja.

Mtaalamu wa vipodozi huhitajika kusafiri nje ya nchi kwa siku kadhaa kila mwaka ili aweze kununua vifaa kwa wingi, na hii huigharimu biashara maelfu ya dola kila mwaka. Ni bidhaa zipi zinaweza kuchapishwa kwa teknolojia ya 3D ili kukidhi mahitaji, na hivyo kuondoa haja ya kusafiri nje ya nchi kila mwaka?

Mifano ya Mafanikio

  • 3D Africa inashirikiana na Afoma, mmiliki wa Hair Wizard nchini Nigeria, kwa kubuni vifaa vya kukausha nywele visivyoungwa kwa nyaya na vinavyoweza kushindiliwa tena nguvu za umeme, vilivyochapishwa kwa njia ya 3D. Badala ya kusafiri kwenda China kila mwaka kununua kwa jumla, yeye hutayarisha bidhaa hizi katika duka lake, kwa kuangazia mahitaji ya wateja wake n ahata kuwauzia wanamitindo wengine.
3D printing africa
Maureen anachapisha mapambo ya vito kupitia teknolojia ya 3D.
  • Maureen, mmiliki wa Afrocentric Afrique nchini Nigeria, hutengeneza samani za kiafrika, shanga, mifuko, mapambo ya ndani mwa nyumba, na vitambaa. Wateja wake ni pamoja na watu binafsi, hoteli, migahawa, na kampuni za ujenzi. 3D Africa ilifanya kazi naye ili kutayarisha mapambo ya vito yaliyochapishwa kwa njia ya 3D kwa kuzingatia mahitaji ya wateja hivyo basi kuibua bidhaa mpya na vyanzo vya mapato.
  • Tochukwu aliunde dawati la kusomea akilenga kufanya kusoma kuwavutie zaidi wanafunzi wa vyuo nchini Nigeria. Kutokana na msaada wa 3D Africa, Tochukwu alishiriki katika tuzo la ubunifu la American Society of Mechanical Engineers (ASME) mjini Nairobi mwaka jana na hivi karibuni ameanzisha kitovu cha uchapishaji cha 3D kwa ajili ya wajasiriamali mjini Lagos.
3D printing africa
Treasure mwenye umri wa miaka 15 ana nia ya kufahamu zaidi uchapishaji wa 3D.
  • Treasure mwenye umri wa miaka 15 yumo katika mpango wa 3D. Anaazimia kujihusisha na kazi zinazoegemea sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati. Kwa sasa, anazidi kubuni na kuchapishia wanafunzi wenzake na familia mapambo ya vito, na sasa anafikiria jinsi ya kutafutia soko bidhaa hizo kwa watu wengine katika jamii yake na hata kuweza kuuza kupitia mifumo ya mtandaoni.

Hitimisho

Uchapishaji kupitia teknolojia ya 3D ni teknolojia ya mabadiliko inayotarajiwa kushuhudia ukuaji mkubwa barani Afrika. Mradi wa 3D Africa utachangia ukuaji huu, kwa hakika. Kimataifa, sekta ya uchapishaji wa 3D inakadiriwa kukua kwa dola bilioni 30 kufikia mwaka wa 2022.