Kutokana na maendeleo makubwa ya benki kwa simu za mkono na intaneti, Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya yametoa tahadhari kwa watumiaji wa simu za mkono kuwa waangalifu ili kujiepusha na ulaghai kwa simu za mkono. Kenya ina asilimia kubwa ya watumiaji wa pesa za simu duniani.
Kampuni kubwa ya simu za mkono nchini Kenya, Safaricom, ambayo ndio mmiliki wa mtandao mkubwa kabisa wa pesa za simu, M-Pesa inawahamasisha Wakenya kuwa waangalifu. Mwezi Juni mwaka huu, kampuni hii ilizindua teknolojia ya "API" ya kuzuia udanganyifu huu. Mwaka jana, mamlaka za Kenya zilitoa wito wa kuwa na juhudi za pamoja za kuzuia ulaghai wa pesa za simu.
Yaliyomo
Hila Zinazotumiwa na Walaghai Kwa Simu za Mkono
Walaghai hutuma ujumbe wa maandishi na wakati mwingine hupiga simu wakijifanya kuwa na watoa huduma kwa wateja toka makampuni ya simu. Kisha wanakuuliza maswali kadhaa na wakati mwingine wanakuuliza neno au namba yako ya siri ili kuweza kupata fursa ya kuingia kwenye akaunti ya simu yako.
Walaghai hawa pia hubadilisha kadi za simu hivyo mmiliki halali wa simu anakuwa hana udhibiti wa kadi yake ya simu. Wafanikiwa kuwa wamiliki wa kadi hiyo, wanaiba fedha zilizoko kwenye akaunti ya namba hiyo. Walaghai wengine huweza hata kuchukua mikopo kutumia kadi yako na kisha kuitupa. Hivyo, ni muhimu kujua jinsi ya kujilinda dhidi ya ulaghai huu. Makala hii itakupa ushauri wa jinsi ya kujilinda.
Nitajilinda Vipi na Ulaghai Kwa Simu za Mkono?
Ni muhimu maelezo yako binafsi yajulikane na wewe tu. Hakikisha wakati wote maelezo hayo hayajulikani na mtu yeyote. Usijibu ujumbe wa simu wa maandishi, barua pepe au simu inayokutaka utoe maelezo yako ya binafsi kama vile namba ya akaunti yako ya benki, tarehe ya kuzaliwa, au namba ya siri ya simu yako. Ikitokea ukapokea ujumbe huo wa ulaghai, piga simu, tuma barua pepe au ripoti wa kampuni yako ya simu na pia ofisi ya "National Cybercrime Management" kwa kutumia namba 0730172700 au incidents@ke-cirt.go.ke.
Hakikisha kuwa namba yako ya siri ni siri yako pekee. Iwe ni namba ya siri ya kadi ya simu au M-Pesa, usimpe mtu yeyote. Hata watoa huduma kwa wateja wa kampuni za simu hawana haki ya kukuuliza namba au neno lako la siri.
Usihifadhi neno lako la siri kwenye zana dijitali kama vile simu au kompyuta. Ni hatari kufanya hivi kwakuwa walaghai wanaweza kutumia mbinu kuingia ndani ya zana hizo na kuiba taarifa ulizohifadhi humo. Simu au kompyuta yako inaweza kuibiwa. Hakikisha utakumbuka neno au namba yako ya siri bila kuhifadhi kwenye zana dijitali.
Kila unapopokea ujumbe unaouliza neno lako la siri, hakikisha unafuta ujumbe huo mara moja. Hii itahakikisha kuwa hutajibu ujumbe kama huo wakati ujao na pia yeyote ambaye atatumia simu yako hatajibu.
Wakati mwingine, unaweza kupokea barua pepe au ujumbe wa maandishi wenye viungo vya intaneti. Usijaribu kubofya kwenye viungo usivyoviamini. Pia, usijisajili kwenye tovuti zisizoaminika kwa kutumia maelezo unayotumia kwenye akaunti yako ya pesa za simu.
Unapotumia "app", hakikisha kuwa umedakua "app" kutoka vyanzo vinavyoaminika. Inamaanisha kuwa utakuwa unatumia "app" sahihi na fedha zako na maelezo yako binafsi vitakuwa salama.
Kuwa makini unapotumia akaunti za mitandao ya kijamii. Usibofye matangazo au viungo vinavyotaka ujiandikishe ili upate huduma za fedha.
Hitimisho
Serikali inahitaji kuelimisha Wakenya juu ya umuhimu wa kuhakikisha maelezo yao ya binafsi ni siri yao. Kwa watumiaji wa huduma ya pesa za simu, ni muhimu uzingatie sheria na masharti ya kampuni ya simu unayoitumia. Ukizingatia ushauri huu, hutakuwa na tatizo na ulaghai wa simu za mkono.
This post is also available in en_US.