Zilipita nyakati ambapo Afrika ilichukuliwa kuwa ya bara lililosahaulika. Katika enzi za kisasa, mengi ya maendeleo yanayoongoza duniani yanatokea bara Afrika. Maeneo ya kazi ya kushirikiana ni mojawapo ya ubunifu huo. Katika siku za karibuni, kumekuwa na ongezeko la maeneo ya ushirikiano ya kufanyia kazi katika masoko ibuka ya ukanda huu.
Kwa wastani, maeneo haya yameongezeka uanachama wao kwa karibu asilimia 50 katika kipindi cha miaka 5. Misri, Afrika Kusini, Nigeria, Kenya, na Morocco ni baadhi ya nchi za Afrika ambazo zinashuhudia kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya maeneo ya kazi ya kushirikiana. Makala haya yataonyesha baadhi ya miundo maarufu katika eneo hili.

Yaliyomo
Je Maeneo ya Kazi ya Kushirikiana ni Nini?
Ni mfumo ambao unaruhusu wataalamu kutoka makampuni mbalimbali ya kufanya kazi wakitumia nafasi moja. Wakodishaji wanaweza kuwa wataalamu binafsi au timu ya wafanyakazi kutoka kampuni chipukizi au hata kampuni zilizoimarika. Mifumo hii ya maeneo ya kufanyia kazi huanzishwa kwa kanuni ya urahisi wa kukidhi mahitaji na gharama nafuu. Baadhi ya maeneo haya hutumika pia kama kitovu cha kampuni chipukizi.
Ofisi za kazi za kushirikiana Afrika Mashariki ni pamoja na Hub255 nchini Tanzania, Impact Hub Kigali nchini Rwanda, na Indigo nchini Kenya.
Manufaa Ya Maeneo Ya Kazi Ya Kushirikiana
- Gharama Nafuu. Matumizi ya maeneo haya huondoa gharama za juu zinazohitajika na wajasiriamali ili kuanzisha kikamilifu ofisi yenye vifaa vyote muhimu. Zaidi ya hayo, hapana haja ya kulipia gharama za huduma nyinginezo kwa vile nyingi ya huduma ni za kwa pamoja. Vilevile, inaruhusu mtumiaji kulipa kila siku, kila wiki, au kila mwezi.
- Kuwezesha mahusiano ya kitaalamu. Maeneo haya hujumuisha watu kutoka nyanja mbalimbali za kitaalamu. Kwa hivyo, mtu anaweza kushirikiana na wataalamu wengine kwa kukamilisha miradi au hata kujifunza ujuzi wa ziada ambao utasababisha ukuaji wake kibiashara au kitaaluma.
- Kuimarisha ukuaji na ustawi. Kutokana na mpangilio usio rasmi katika maeneo haya ya kazi ya kushirikiana, wafanyakazi wanapata fursa ya kufanya kazi bila kupata uchovu wa akili unaohusishwa na ofisi za kawaida. Isitoshe, utafiti mbalimbali umeonyesha kuwa takriban asilimia 90 ya watu katika mazingira ya kazi ya ujamaa huwa wamefurahi zaidi ikilinganishwa wakiwa katika ofisi ya kawaida.
Huduma Zinazotolewa Katika Maeneo ya Kazi ya Kushirikiana
Maeneo ya kazi ya kushirikiana kutoa huduma za kipekee kwa wakazi. Hata hivyo, kwa kawaida huduma za msingi zinazotolewa huwa kama vile kiti na dawati, uwezo wa kutumia jikoni na vifaa muhimu vilivyomo, huduma za chumba cha mikutano, mtandao thabiti, eneo la mapokezi la pamoja, ikiwa ni pamoja na vifaa vya pamoja kama mashine za kupiga chapa, mdaki na kinukuzi.
Zaidi ya hayo, usimamizi wa maeneo haya unaweza kutoa huduma za ziada kwa wapangaji wake wote au wale waliojisajili kupokea huduma za ziada kwa gharama ya juu. Kwa hivyo, ni muhimu kutathmini huduma zote zinazotolewa na maeneo ya kazi ya kushirikiana kabla ya kutia sahihi mkataba. Baadhi ya huduma za ziada ni pamoja na:
- Upatikanaji wa ofisi. Baadhi ya maeneo ya hutoa dawati na kiti pamoja na ofisi funge.
- Uwekaji wa nembo ya kampuni yako. Kulingana na wasimamizi wa maeneo haya au ada iliyolipwa, unaweza kupata nafasi ya kuweka bango la kibiashara kwenye jengeo hilo.
- Muda wa kufanya kazi. Hakikisha kuuliza kuhusu muda wa kufungua na kufunga ili pasiwepo usumbufu iwapo una nia ya kuanza kazi mapema sana asubuhi au kufanya kazi hadi usiku.
- Usalama. Kila mtu anataka kufanya kazi katika mazingira salama. Kabla ya kusaini mkataba wa kukodisha, ni muhimu ufahamu kuhusu hatua zilizopitishwa za usalama.
Maeneo Maarufu Ya Kazi Ya Kushirikiana Barani Afrika
Ingawa kuna orodha ndefu ya sehemu hizi katika ukanda huu, makala haya yatazungumzia baadhi ya zile maarufu. Hii ni pamoja na:
Nairobi Garage (Kenya)
Nairobi Garage ni mojawapo ya maeneo aanzilishi ya ushirikiano wa kufanya kazi nchini Kenya. Inapatikana katika vitongoji kwasi vya Westlands na Kilimani. Hutoa huduma zake kupitia mpango wa ofisi wazi na vilevile ofisi za kibinafsi. Wapangaji pia wana fursa ya kutumia nafasi wazi ya kufanyia matukio na vilevile chumba cha mikutano. Mtu anaweza kujichagulia mpango wa malipo funge, wa malipo rahisi, au wa malipo ya kila siku. Wadhibiti wa maeneo haya pia huandaa warsha, utambulisho wa wawekezaji, jamii ya mtandaoni kupitia wavuti, na msaada wa matangazo na mwonekano. Sehemu hii huwa wazi kila siku za wiki 8:00-17:30.
- Eneo: M2 Mirage Towers Westlands, gorofa ya 8 Pinetree Plaza Kaburu Drive Ngong Road
- Gharama: KES 2000 kila siku au KES 20,000 kila mwezi (dawati la kukodi watu wengi), KES 25,000 kila mwezi (dawati la mtu mahsusi)
- Mawasiliano: westlands@nairobigarage.com / ngongroad@nairobigarage.com
33B Workspace (Nigeria)
33B Workspace inalenga wafanyakazi huria na biashara ndogo ndogo mjini Lagos. Hutoa huduma zenye gharama nafuu na maeneo ya kazi yenye vifaa kikamilifu. Huduma ni pamoja na chumba cha mikutano, ofisi halisia, na ofisi za kibinafsi. Kwa kawaida hufunguliwa kati ya Jumatatu hadi Ijumaa baina ya 07:00-18:00.
- Eneo: 33B Adebayo Doherty Road Lekki Phase 1, Lagos
- Gharama: Naira 120,000 kila mwezi
- Mawasiliano: info@33b.com.ng
Cape Town Office (Afrika Kusini)
Cape Town Office imekuwepo tangu mwaka 2011 na ni mojawapo ya sehemu za hadhi ya juu za maeneo ya kazi ya kushirikiana kimataifa. Huduma zake ni pamoja na upatikanaji wa nafasi saa ishirini na nne kwa juma, vyumba vya mikutano ambayo vina televisheni za kisasa, mikutano ya kila mwezi ya kufahamiana, na wanachama wa mtandaoni ikiwa ni zaidi ya washiriki hai 300. Mtu anaweza kupata dawati maalum, ofisi ya kibinafsi, au mahali spesheli pa kukaa na eneo wazi la kazi kwa idadi fulani ya saa kila mwezi. Kila kitengo cha huduma kina vipengele maalum.
Eneo: 62 Roeland Street, 2nd & 3rd floor, Gardens, 8001, Cape Town
Gharama: Kitengo cha chini huanzia R1600 kila mwezi bila gharama ya ushuru
Jinsi ya kuwasiliana: lizelle@capetownoffice.com
Hitimisho
Sawa na maeneo mengine duniani, Afrika imeshuhudia ongezeko kubwa ya maeneo ya kazi ya kushirikiana. Sehemu kama hizo huvutia wafanyakazi huria mbalimbali, biashara chipuzi, na hata kampuni zilizojiimarisha vizuri. Iwapo unatafuta sehemu ya kukodi katika mazingira kama hayo, hakikisha kuwa umejua kuhusu huduma wanazotoa ili kubaini iwapo zinaafika mahitaji yako binafsi na ya kitaaluma.