Taifa la Kenya limeorodheshwa nafasi ya sita kwa idadi kubwa ya vijana wanaoshiriki kucheza kamari barani Afrika huku mitandao ya kamari na michezo ikiongoza usakuraji wa Google nchini Kenya mwaka wa 2018. Zaidi ya vijana 500,000 wameorodheshwa kama wadeni kupitia kwa Shirika la Kumbukumbu za Mikopo (CRB) kwa kutoweza kulipia madeni yao. Mikopo mingi iliyochukuliwa na vijana ni kwa madhumuni ya kamari.
Sababu za msingi za ongezeko la shughuli za kamari ni pamoja na kiwango kikubwa cha mpenyezo wa kidijitali, uvumbuzi wa malipo ya simu kama vile M-Pesa, idadi kubwa ya vijana, ukosefu wa ajira na kutamauka kwa jinsi ya kujikimu maishani kwa Wakenya wengi. Kutokana na ongezeko la kampuni za mikopo za mtandaoni na kampuni za uchezaji kamari, wengi wa vijana wametekwa katika uraibu wa kamari. Serikali inapania kudhibiti kampuni za kamari ili kusaidia kuopoa hali hii.
Yaliyomo
Kampuni Kuu za Kamari Nchini Kenya
Katika siku za karibuni, kumekuwa na ongezeko la idadi ya maeneo ya kuchezea kamari. Kuna zaidi ya kampuni 30 zinazojihusisha na shughuli za kamari nchini Kenya.
Kampuni tofauti huwa na viwango tofauti vinnavyoambatanishwa na utakachotuzwa. Hivyo basi, mafanikio ya mtu humhitaji ateue viwango bora zaidi. Ikiwa matokeo ya michezo ni kama ulivlivotabiri, basi utakuwa mshindi. Vilevile, kama ni kinyume cha matukio, unapoteza pesa ulizoekeza. Kwa kuangalia viwango kutoka tovuti mbalimbali unaweza kuihakikishia ushindi.
Shinikizo Kwa Kampuni za Kamari
Kutokana na ongezeko la idadi ya kampuni za kamari, serikali imeweka mikakati ya kulinda Wakenya dhidi ya uraibu wa kucheza kamari na dhuluma inayoandamana na shughuli hizo. Bodi ya Kudhibiti na Kutoa Leseni ya Kamari (BCLB) kupitia benki na wadhibiti wengine wa uhamisho wa fedha wamefanya iwe vigumu kwa watu kutoa na kuhifadhi fedha kwenye mitandao ya kamari. Awali, tumeona leseni za baadhi ya kampuni za kucheza kamari zikifutiliwa kwa kushindwa kulipia ushuru unaohitajika. Hata hivyo, kesi zimekuwepo kwa muda na zimeweza kutatuliwa kupitia mahakama. Kwa mujibu wa hoja ya hivi karibuni, serikali imekataa kutoa upya leseni za kampuni hizi za kucheza kamari ili kuhakikisha kuwa (kampuni hizo) zinaangazia kanuni zilizowekwa na BCLB.
Aprili 1, Waziri wa Mambo ya Ndani na Uratibu wa Serikali ya Taifa Dkt. Fred Matiang’i alitahadharisha kuwa kampuni hizi za kucheza kamari zitarajie hatua kali. Alisema kuwa sekta hii ilichangia kuwapotosha vijana wengi. Baraza la Usalama la Taifa pia liliridhia kauli hiyo. Halmashauri hiyo pia inachunguza athari na vitisho vinavyoambatana na uchezaji kamari nchini kama vile utakatishaji fedha.
Kampuni za kamari zilipewa makataa ya hadi 1 Julai 2019, ili kukidhi masharti mapya ya shughuli za kamari. Baadhi ya masharti yaliyohitajika kuafikiwa ni pamoja na kuthibitisha kuwa walikuwa wanaendesha biashara kwa mujibu wa sheria. Pia, walihitajika kuonyesha kuwa walikuwa na uwezo na utaratibu mzuri wa kifedha kwa miaka minne iliyopita.
Tangu kutiwa kwa shinikizo, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru ya Kenya (KRA) imekagua na kuruhusu kampuni kumi za kucheza kamari ambazo leseni zake zilikuwa zimefutiliwa kutokana na kutofuata sheria za ushuru. Kampuni hizi ni pamoja na Bet Boss, Betway, OdiBets, Mozzartbet, Ken Bookmakers, Palms Bet, Eastleighbet, Lucky 2u, Kick Off na Eazi Bet. Leseni za kampuni 27 hazikutolewa upya kwa kushindwa kukidhi masharti hayo. Baadhi ya kampuni ambazo leseni zake hazijatolewa upya ni pamoja na Betin, Bet Boss, Betway, Palmsbet, Betpawa, Atari Gaming, World Sports Bet, Premierbet, World Sports Bet, Defa Bet, na 1xbet.
Mapema mwaka huu, BCLB ilitangaza sheria mpya ya kupiga marufuku matangazo ya mabango ya kamari, matangazo ya kamari kwenye mitandao ya kijamii, matangazo ya kamari baina ya saa kumi na mbili asubuhi hadi saa nne usiku na kuidhinishwa kwa shughuli za kamari na watu mashuhuri. Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Kenya ilifutilia sharia hizo.
Serikali ya Kenya imeanzisha upya Mswada wa Kamari 2019 ambao unapendekeza ada mpya, sheria ya umiliki na ufuatiliaji wa shughuli hizi za kamari.
Ni nini cha Ziada, Mbali na Kukusanya Ushuru
Inakadiriwa kuwa sekta ya kamari inazalisha mapato ya bilioni 200 kila mwaka. Katika mataifa mengi, ushuru unaotozwa kwa kila ushindi, kawaida huwa chini ya asilimia ishirini. Nchini Kenya, ushuru unaotozwa kwa kila ushindi katika sekta ya kamari ni asilimia 35. Serikali ya Kenya ipo katika njia panda; baina ya kukusanya mapato na kuwalinda vijana. Serikali haipaswi tu kutumia utozaji wa ushuru kama njia ya kudhibiti kamari ila kwa kutafuta njia nyinginezo za kuhakikisha kwamba vijana hawatekwi na jinamizi la kushikiri michezo ya bahati nasibu.
Miongoni mwa mbinu ambazo serikali inaweza kutumia ili kupunguza uraibu wa kamari ni kupiga marufuku kutumia mabango kwa kudhamini matangazo.
Hitimisho
Serikali ina jukumu ya kuwalinda raia wake dhidi ya unyonyaji na kuzingatia kuwawezesha vijana kujikimu. Hatua ya kukusanya ushuru wa juu kutoka kwa kampuni za kamari kutaendeleza zaidi kamari. Kutokana na hatua kama hiyo, kampuni hizi za kamari zitalazimika kuwanasa watu zaidi ili washiriki uchezaji kamari ili kuzidisha mapato yao na faida.