Wanamuziki Tajiri Zaidi Nchini Kenya na Kile Tunachoweza Kujifunza Kutoka Kwao

Tafsiri:
en_US

Awali, idadi kubwa ya Wakenya waliuona muziki kama aina ya burudani tu ambayo mtu huweza kushiriki katika kipindi chake cha mapumziko. Baada ya kuona jinsi wasanii wengi wengi walivyokuwa maskini, wazazi wengi hawakuruhusu watoto wao kujihusisha na usanii kama kazi. Kwa bahati nzuri hali imebadilika. Watu binafsi wenye vipaji sasa wanaendesha maisha yao kutokana na sanaa mtandaoni na nje ya mtandao.

Vijana wengi wenye ndoto za kuwa wanamuziki wanajitahidi kufikia maisha ya kifahari ambayo ni sawia na wanamuziki mashuhuri kama Jay Z, Beyoncé, Davido, na Wiz Kid. Hata hivyo, mafanikio hayo hayaji kwa urahisi. Kuna baadhi ya kanuni ambazo wasanii chipukizi wanahitajika kuangazia ili kutimiza malengo yao. Kwa hivyo, makala haya yatazungumzia kuhusu wanamuziki tajiri wa Kenya na yale tunayoweza kujifunza kutoka kwao.

1. Sauti Sol

how to make money from music in kenya
Sauti Sol ni mojawapo ya kundi la wasanii wa Kenya ambao wamepata utajiri wao kupitia muziki.

Ukimuuliza mtu yeyote ambaye anasikiliza wasanii wa kisasa wa Kenya, pana uwezekano mkubwa kuwa jina la Sauti Sol litakuwa la kwanza kutajwa. Hii ni bendi ya wavulana barobaro ambayo imeundwa na wanamuziki wanne wenye vipaji: Savara Mudigi, Bien-aime Baraza, Wilis Chimano, na Polycarp Otieno. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005, kikundi hiki kimejijengea sifa nchini na kimataifa.

Kwa miaka iliyopita, wamepata tuzo mbalimbali kuu na uteuzi ikiwa ni pamoja na MTV Europe Music Award, tuzo za Channel O Music, Kisima Award, na tuzo za BET. Zaidi ya hayo, wao wameshirikiana na wasanii wenye haiba kama vile Tiwa Savage, Burna Boy, na Patoranking.

Mafanikio ya kikundi hiki hayakutokea mara moja, swala ambalo wanamuziki chipukizi wa Kenya wanapaswa kutambua. Mojawapo wa yale tunaweza kujifunza kutokana na kazi ya mafanikio ya Sauti Sol ni umuhimu wa kudumisha mahusiano ya kitaalamu. Licha ya vijana hawa kuwa wenye vipaji, wanaelewa kwamba ujuzi pekee hautawanufaisha katika sekta hii yenye ushindani.

Kwa kuwa na timu bora ambayo inajumuisha meneja, msemaji, na wataalamu wengine muhimu, wasanii hawa wameonyesha kuwa wameuchukulia muziki kama kazi na wala si kazi mbadala. Wasanii chipukizi wa Kenya wanapaswa kufahamu kwamba hawawezi kuwajibikia shughuli zao zote wenyewe. Kwa kubuni timu ya usimamizi, inakuwa rahisi kwa msanii kuzingatia muziki wake wakati watu wengine wakiyashughulikia maswala mengineyo.

2. Bahati

top kenyan richest musicians
Bahati ni mmoja wa wanamuziki tajika wa injili nchini Kenya.

Mwanamuziki mwingine tajiri nchini Kenya ni Bahati. Alianza usanii wake mwaka 2012 na ameishia kuwa mmoja wa wasanii maarufu wa kisasa nchini. Hadithi yake ni moja ambayo watu wengi katika taifa hili la ulimwengu wa tatu wanaweza kujihusisha nayo. Alibakia yatima katika umri mdogo na alilazimika kuhamia kwa mojawapo ya makazi ya mayatima katika moja ya makazi duni ndani ya mji mkuu wa nchini. Hadithi yake inaweza kuyasisimua matumaini ya wanamuziki chipukizi ambao wana historia inayofanana na yake. Kwa kweli, mtu anaweza kutumia hali yake ya sasa kama msukumo wa kuboresha kesho yake kuliko kuiona kama hatima yao.

Kanuni nyingine tunayoweza kujifunza kutokana na Bahati ni kuwepo na haja ya kutumia wafuasi wako kujipatia wafuasi hata wengi zaidi. Wengi wa wasanii wanaochipuka nchini Kenya hulenga kilele cha usanii kuwa magari ya kifahari, kusafiri mataifa mengi ya kigeni, na kupata hadhi kutokana na umaarufu. Huku maisha hayo yakionekana kuwa mazuri, ni muhimu “kuchumia juani uje ule kivulini.”

Bahati ameashiria welewa tosha kwa kuzidisha faida kutokana na hali yake ya sasa, dhana ambayo wanamuziki wengine wa Kenya wanapaswa kuiga. Baada ya kutambua kwamba ana mashabiki wengi nchini kote, alijianzishia kipindi cha televisheni kiitwacho Bahati Reality. Mbali na kuwa chanzo kingine cha mapato, kipindi hiki kimekuwa nyenzo ya kujitangaza na hivyo kuishia kupata mikataba ya ufadhili kama vile Zoe Lotion na simu ya Vivo.

3. Akothee

Akothee, ambaye pia anaangaziwa kama mpenda starehe, bila shaka ni mmoja wa wanamuziki tajiri zaidi wa kike nchini Kenya. Hadithi yake ya ufanisi imejengwa kwa ujasiri na jitihada. Aliolewa kabla ya kukamilisha masomo yake ya sekondari. Alipohitimu miaka 17, alikuwa na ujauzito na watoto 4 ingawa mmoja aliaga dunia angali mchanga. Wakati fulani, aliwahi kufanya kazi kama mchuuzi wa samaki na baadaye kama dereva teksi ili aweze kukidhi mahitaji ya watoto wake.

Hii leo, anamiliki magari kadhaa na nyumba za kifahari. Bidii yake katika sekta ya muziki imefanya akashirikiana na wasanii tajika kama Diamond Platinumz na Flavor. Isitoshe, amejizolea tuzo za kifahari ikiwa ni pamoja na tuzo mbili za AFRIMMA na African Entertainment Awards, Marekani. Funzo kutokana na haya ni kuwa: JARIBU HADI UFAULU!

Jambo jingine ambalo wasanii chipukizi wa Kenya wanaweza kupata kutokana na maisha ya kitaaluma ya Akothee, ni kuwepo kwa haja ya kuwekeza kwa njia ya busara. Kwa wastani, wanamuziki wa Kenya hufikia kilele cha usanii wao kwa muda wa miaka 5-10. Hii ni kutokana na hali ya ushindani mkubwa wa sekta na hamu ya watazamaji kuona wasanii wapya mara kwa mara. Hivyo basi, ni muhimu kwa msanii kuyawekeza mapato yaliyopatikana na mustakabali wake kutoka kwa muziki na shughuli nyinginezo.

Akothee alifanya yayo hayo na kwa sasa anajichumia pato kubwa. Alitumia mapato yake na kuanzisha Akothee Property (kampuni inayojihusisha na mali isiyohamishika) na Akothee Safaris (biashara ya usafiri). Hatua hizi za kimkakati ndizo zinamfanya awe mmoja wa wanamuziki tajiri sana nchini Kenya.

4. Willy Paul

top richest musician in kenya

Fauka ya utata unaoandamana naye, Willy Paul amejihakikishia nafasi katika orodha ya wanamuziki tajiri zaidi nchini Kenya. Kama ilivyo na wasanii wengi wenye vipaji nchini Kenya, maisha yake ya wali yalikuwa ya changamoto tele. Alizaliwa na seremala na msusi na kukulia katika mazingira magumu katika mtaa wa makazi duni wa Mathare. Kifo cha baba yake kilimsababisha kuacha shule na kuanza kushiriki katika kazi mbalimbali ili aweze kuwasaidia ndugu zake na mamake aliyekuwa akiugua.

Kama kuna jambo moja ambalo wanamuziki chipukizi wa Kenya na vijana kwa ujumla wanaweza kjifunza kutokana na alivyoanza Willy Paul na hali yake ya sasa ni kwamba awali yako haipaswi kuizuia ndoto yako. Kama Willy Paul angesalia kujijutia kuhusu kushindwa kwake kukamilisha elimu ya sekondari au changamoto zake nyinginezo za maisha, basi jina lake na ubunifu wake haungejulikana zaidi ya makazi duni ya Mathare.

Nyimbo zake zimeweza kutambuliwa hadi kimataifa. Kwa mfano, kuna video mbalimbali kwenye Youtube zinazoonyesha wimbo wake ‘I do’ ukichezwa katika harusi duniani kote. Amewashirikisha wasanii mashuhuri wa kimataifa kama vile Alaine na Ce’cile. Ni wazi kwamba dhamira yake ya kutojifunga na hali yake ya awali ya umaskini imechangia umaarufu wake na utajiri anaoufurahia kwa sasa.

Matumizi yake ya kimikakati ya mitandao ya jamii, ni sehemu nyingine ambayo wasanii wanaochipuka nchini Kenya wanapaswa kuiga. Ana wafuasi milioni 1.2 kwenye Instagram na zaidi ya 350,000 katika Facebook. Pia anatumia majukwaa ya kidijitali kama vile Mdundo, Youtube, na Spotify kuuza muziki wake. Wanamuziki wachanga nchini Kenya ambao wanatumia mikakati kama hii wanaweza kuingia katika orodha hii ya wanamuziki tajiri zaidi nchini Kenya.

Kenyan artists using digital platforms to increase their income
Willy Paul hutumia njia za kidijitali kuuza muziki wake.

5. Jaguar

wealthiest kenyan musicians

Safari ya Jaguar ni hadithi inayohusu kutoka chini kwa tambara bovu hadi hadhi ya utajiri. Kama vile walivyo watu wengine wengi katika nchi hii ya ulimwengu wa tatu, familia yake ilikuwa maskini. Anakumbuka jinsi mara nyingi alilazimika kulala kwenye magari ya umma (matatu) kwa ajili ya ukosefu wa makazi bora. Baada ya kumaliza elimu yake ya msingi, alianza kuosha magari kama njia ya kupata riziki.

Hasa, hakuziruhusu changamoto hizi kuufafanua mustakabali wake. Alifanya kazi kwa bidii na kutumia talanta yake ili kufanikiwa katika sekta ya muziki nchini Kenya. Mwanamuziki huyu, ambaye pia ni mbunge wa eneo la Starehe, amefanya kazi na wasanii maarufu kama vile Mafikizolo na Iyanya. Jaguar amepokea tuzo na teuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na East Africa Music Awards, Nzumari Awards, na Channel O Music Video Awards.

Mojawapo ya mambo ya msingi ambayo wasanii wanaoibuka wa Kenya wanapaswa kujifunza kutoka kwa Jaguar ni kuwa na utamaduni wa kuwa na akiba ya fedha. Licha ya kwamba anaishi maisha ya kifahari yanayohusisha magari ya kifahari na safari ghali, yeye daima hujibidiisha kuwekeza mapato yake yanayotokana na muziki. Katika baadhi ya vyombo vya habari alipowahi kuhojiwa, ilibainishwa kuwa Jaguar “husisitiza sana kuhusu kuweka akiba. Anasema kuwa hata mabilionea huweka akiba, lau sivyo, watafilisika. ” Hili ni jambo moja dhahiri amabalo wasanii wote wa Kenya wanastahili kulikumbatia.

Hitimisho

Katika muongo uliopita, sekta ya muziki nchini Kenya imekua kwa kiasi kikubwa. Kuna wasanii wengi ambao walipata wafuasi wengi humu nchini na kimataifa. Hata hivyo, wengi wa wanamuziki maarufu hawana mengi ya kuonyesha kutokana na ufanisi huu. Kwa kuangazia wanamuziki tajiri zaidi wa Kenya inaonyesha kuwa kuna kanuni kadhaa na mikakati ambayo inaweza kuwasaidia wasanii chipukizi ili kuangaza mustakabali wao.