Mara nyingine, waweza kujikuta ukihitaji pesa haraka ili kutatua jambo fulani. Waweza kuwaendea marafiki au ndugu ili wakusaidie. Lakini yawezekana wasiwe katika nafasi ya kukusaidia. Kwa bahati nzuri, waweza kuomba mkopo kutoka benki au huduma ya mtandaoni ya kukopesha pesa. Licha ya benki, maeneo yafuatayo waweza kuyatumia kupata mikopo binafsi ya biashara.

Mikopo Binafsi ya Biashara

M-Shwari

M-Shwari ni huduma ya kibenki isiyotumia karatasi inayotolewa kupitia M-Pesa. Ni ushirikiano ulioanzishwa mwaka 2012 kati ya Safaricom na benki ya CBA. Wateja wa Safaricom, sasa wanaweza kukopa mkopo kutoka M-Shwari. Ili kupata mkopo huu, yakubidi uwe na umri wa miaka 18 au zaidi, uwe na akaunti hai na iliyosajiliwa ya M-Pesa kwa kipindi cha miezi sita. Yakubidi pia uwe na menyu iliyohuishwa ya M-Pesa.

Kiwango cha chini cha mkopo unachoweza kukopa ni shilingi 100 za Kenya wakati kiwango cha juu ni shilingi 20,000 za Kenya. Mkopo una muda wa marejesho wa siku 30, ukiambatana na riba ya asilimia 7.5. Waweza kulipa mkopo moja kwa moja kwa kupitia akaunti ya M-Pesa. Iwapo siku thelathini zitakwisha ukiwa hujalipa mkopo, wanakata deni kutoka M-Shwari yako. Unapochelewesha malipo, unalipa deni pamoja na gharama ya ziada ya asilimia 7.5 ya salio lako.

KCB M-Pesa

Hii ni akaunti ya kuweka na kukopa Ni matokeo ya ushirikiano kati ya Safaricom na Benki ya Biashara ya Kenya (KCB). Kiwango cha chini mtu awezacho kukopa ni shilingi 10 za Kenya wakati ambapo kiwango cha juu ni shilingi 1,000,000 za Kenya. Unahitaji kuamilisha akaunti yako ya KCB M-Pesa. Ili kukidhi masharti ya mkopo, ni lazima uwe na umri wa miaka 18 au zaidi, uwe na akaunti hai na iliyosajiliwa ya M-Pesa kwa kipindi cha miezi sita pamoja na menyu iliyohuishwa ya M-Pesa. Matumizi yako ya nyuma ya M-Pesa, itaamua kiwango unachoruhusiwa kukopa.

MCop-Cash

MCop-op Cash ni mkopo utolewayo na Benki ya Ushirika ya Kenya. Kwa kutumia program tumizi ya MCop-op, waweza kupata huduma za kibenki kama mikopo. Kiasi cha chini unachoweza kukopa ni shilingi 3,000 za Kenya na shilingi 100,000 za Kenya kama kiasi cha juu.

Ili kukidhi masharti ya mkopo, yakubidi uwe mteja wa Benki ya Ushirika. Wahitajika pia kupakua program tumizi kutoka stoo ya Google au iOS. Mkopo unaambatana na gharama zifuatazo:
Mkopo binafsi wa mwezi mmoja una riba ya asilimia 1.166 wakati ule wa miezi mitatu riba ni asilimia 3.498. Mkopo wa biashara una riba ya asilimia 1.166 wakati mkopo wa bima wa miezi mitatu, riba yake ni asilimia 0.102.

Eazzy Loan

Eazzy Loan ni bidhaa itolewayo na Benki ya Equity. Unahitajika kuwa na akaunti hai ya benki ya Equity. Pia unahitaji kuwa na laini ya simu ya mtandao wa Equitel katika simu yako ya mkononi. Kuna aina mbili za mikopo uwezayo kupata. Mkopo wa benki ya Equity na Eazzy Loan.

Waweza kukopa hadi shilingi milioni tatu za shilingi ya Kenya. Kiwango cha chini cha mkopo wa benki ni shilingi mia moja ya Kenya na cha juu ni shilingi laki mbili za Kenya.

Mkopo wa benki una miezi kumi na mbili ya marejesho wakati Eazzy Loan ni kipindi cha miezi thelathini ya marejesho. Mikopo hiyo ina riba kati ya asilimia mbili na kumi, ikijumuisha gharama za benki, ada ya uidhinishaji mkopo na kodi ya serkali.

Branch

Branch ilianzishwa rasmi mwaka 2015, ikiwa na makao yake mjini San Fransisko na ofisi jijini Nairobi. Wakenya wengi wamekuwa wakikopa mikopo kutoka huduma hii. Ili kukidhi kupata mkopo kutoka Branch, unahitajika kuwa mtumiaji wa M-Pesa na kuwa na akaunti ya Facebook inayolandana na majina yako halisi kwenye kitambulisho chako.

Waweza kuipakua program tumizi kutoka stoo ya Google na kisha kuiunga na akaunti yako ya Facebook. Kisha jaza taarifa zihitajiwazo kama vile nambari yako ya simu. Programu tumizi ina kiwango cha chini cha mkopo cha shilingi 1,000 za Kenya na shilingi 50,000 za Kenya kama kiwango cha juu. Mkopo wa awali unatolewa kupitia M-Pesa, wakati kiwango cha riba kinategemea muda wa marejesho.

Tala

Tala ilianzishwa rasmi mwaka 2014, zamani ilijulikana kama Mkopo Rahisi. Ili kupata huduma ya Tala, unatakiwa uwe na rekodi nzuri ya matumizi ya M-Pesa na pia uwe na simu janja. Kiwango uruhusiwacho kukopa, kinategemea na urejeshaji wako wa mkopo pamoja na miamala ya M-Pesa.

Unachotakiwa kufanya ni kupakua programu tumizi ya Tala kutoka stoo ya Google na kuiunga na akaunti yako ya Facebook. Kisha jaza taarifa zihitajiwazo. Kiwango cha chini cha mkopo ni shilingi 500 za Kenya huku kiwango cha juu kikiwa ni shilingi 50,000 za Kenya pamoja na riba ya asilimia 15. Mkopo una uchaguzi wa awamu za wiki tatu kupitia M-Pesa.

Timiza

Timiza ni program tumizi iliyozinduliwa hivi karibuni na benki ya Barclays. Bidhaa hii inapatikana kwa mtu yeyote mwenye simu ya mkononi na hivyo si lazima kuwa na akaunti ya benki ya Barclays ili kupata mkopo. Waweza kuitumia programu tumizi hii kutunza pesa kwa kuziweka kwenye akaunti yako ya M-Pesa ili kupata mkopo zaidi. Waweza pia pata bidha hii iwapo huna simu janja kwa kupiga *848# kwa kutumia simu yako ya mkononi.

mKey

Finserve Africa ilianzisha programu tumizi ya mKey kama mapinduzi ya huduma ya kifedha inayomjali mteja. Kwa kutumia programu tumizi hii, unaweza kutuna fedha kwenye mikoba kama vile M-Pesa, Equitel pesa na Airtel pesa. Unaweza pia kununua muda wa kuongea kwenye simu zilizosajiliwa na Safaricom, Equitel, Airtel, Telkom na Faiba. Licha ya kukopa kupitia mKey, unaweza pia kulipia bidhaa na huduma.

Hitimisho

Kabla ya kutumia huduma tulizoorodhesha hapo juu, hakikisha kuwa unajua kiwango cha riba, kipindi cha malipo, na masharti ya mkopo.