Mafunzo Muhimu kwa Bara la Afrika Kutoka kwa Mshindi wa Tuzo la Nobel, Esther Duflo

Tafsiri:
en_US

Esther Duflo ni mchumi Mmarekani aliyezaliwa Paris, Ufaransa tarehe 25 Oktoba 1972. Yeye ni Profesa wa Kupunguza Umaskini na Maendeleo ya Uchumi katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT). Esther Duflo amekuwa sasa mwanamke mwenye umri mdogo na pia mwanamke wa pili kuwahi kushinda Tuzo la Nobel la Uchumi, kwa ajili ya kazi yake ya njia ya majaribio ili kupunguza umaskini duniani. Haya ni baadhi ya mambo muhimu ambayo bara la Afrika linaweza kujifunza kutokana na mwanauchumi huyu shupavu.

poverty alleviation africa
Esther Duflo amekuwa sasa mwanamke mwenye umri mdogo na pia mwanamke wa pili kuwahi kushinda Tuzo la Nobel la Uchumi.

Njia Bora ya Kutatua Tatizo ni Kulifanyia Majaribio

Esther Duflo anasema kuwa ili kupambana na tatizo, unahitaji kukabiliana nalo hatua kwa hatua. Anapendekeza kuwa usijaribu kutumia dhana yako, badala yake, jaribu kuyaleta mawazo ya kisayansi. Yafanye majaribio na bila shaka utaishia kuwa na suluhisho kamili.

Kuboresha Mifumo ya Elimu

Kutokana na majaribio ya kubahatisha yaliyofanywa na Esther na wenzake, Waafrika wanapaswa kufahamu kuwa, ili kuboresha matokeo, inastahili kuambatanisha mafunzo yanayolingana na kiwango cha uelewa cha wanafunzi badala ya kuegemea umri.

Majaribio yalionyesha kwamba masomo duni miongoni mwa watoto wa shule magharibi mwa Kenya haiyakuwa kwa sababu ya uhaba wa vitabu vya kiada au hata baa la njaa. Masomo yanaweza kuboreshwa kwa kutekeleza vipindi vya ziada na kuanzisha programu za kimafunzo kupitia kompyuta shuleni. Jambo hili litaweza kushughulikia mahitaji ya wanafunzi dhaifu ili waweze kufana. Majaribio sawia yalifanyika nchini India, na matokeo yalikuwa yayo hayo.

Jaribio jingine lilifanywa na Duflo na Michael Kremer nchini Kenya linaonyesha kwamba, kwa kupunguza tu idadi ya wanafunzi wanaofunzwa na walimu wa kudumu hakuboreshi ufunzaji. Hata hivyo, kuwahusisha walimu kwa njia ya mikataba ya muda mfupi na kuifanywa upya tena wakiafikia matokeo mazuri kunaleta matokeo mazuri. Ubora wa shule pia lazima uangaziwe ili kupata wanafunzi zaidi shuleni.

Kukumbatia Teknolojia ya Kisasa Katika Kilimo

Swali kuu hapa lilikuwa, ni kwa nini wakulima wadogo barani Afrika mara nyingi hushindwa kutumia teknolojia ya juu kama vile mbolea? Hii ni licha ya hata kwamba huwa ni rahisi kutumia, na faida yake huwa ni ya kipekee.

Majaribio ya kina ya nyanjani yalifanywa na Esther na wenzake magharibi mwa Kenya. Waligundua kuwa wakulima walikuwa wakiathirika kutokana na upendeleo uliopo kwa sasa. Wakulima walionekana kuangazia faida ya muda mfupi kama muhimu kushinda yale ya muda mrefu. Wakulima waliopendela manufaa ya sasa waliupuuzilia mbali uamuzi wa kununua mbolea kwa bei nafuu na kusubiri hadi muda mfupi tu kabla ya dakika za mwisho. Wakulima hao huishia kutonunua mbolea kwa sababu hawapendi kiasi kidogo cha akiba cha siku zijazo ikilinganishwa na kiasi kikubwa zaidi cha mapato.

Majaribio ya Esther yalionyesha kuwa wakulima walinunua mbolea zaidi iwapo ingetolewa kwao kwa kipindi kifupi cha kipunguzo, mapema katika msimu wa kupanda kuliko katika kipunguzo kikubwa zaidi bila kikomo (makataa). Ruzuku ya muda kwa mbolea ni bora zaidi ikilinganishwa na ruzuku ya kudumu. Wakulima wa Afrika wanapaswa kukumbatia somo hili kubwa na hi itaimarisha sekta ya kilimo na kuiweka katika ngazi za juu.

Upatikanaji wa Mikopo Kupitia Mipango ya Mikopo Midogo

Esther Duflo alitekeleza mradi nchini Morocco ili kutathmini matokeo ya miradi ya mikopo midogo. Alizamia katika maeneo ya vijijini huko Morocco, ambapo pana upungufu wa upatikanaji wa mikopo rasmi. Kutoa mikopo kwa familia zenye kipato cha chini kuna uwezo wa kuongeza uwekezaji katika afya na elimu.

Mikopo midogo ilichangia kuongezeka kwa mauzo, matumizi nyumbani, na faida katika vijiji. Ongezeko hili linaonyesha kwamba programu hizi zinastahili kuenezwa hadi katika maeneo mengi ya vijijini barani Afrika, na hii itaboresha hali ya maisha ya watu .

Kuboresha Afya na Dawa

mobile clinic health
Kliniki tamba nchini India.

Afrika inapaswa kujifunza kutokana na nchi nyinginezo. Duflo, vilevile, alifanya majaribio nchini India kuhusu jinsi ya kuanzishwa kwa kliniki tamba kuliongeza kiasi cha chanjo kwa watoto. Katika nchi za Afrika, kutofika kazini kwa wahudumu wa afya pamoja na huduma mbovu katika vituo vya afya huzizuia familia maskini kupokea chanjo.

Kwa kuanzishwa kliniki tamba nchini India ili kutoa chanjo kulipelekea kuongezeka kwa viwango vya chanjo kwa zaidi ya mara sita. Nchi za Afrika zinapaswa kujifunza kutokana na hili ili kuboresha afya katika familia zenye kipato cha chini.

Esther Huwatia Moyo Wanawake

Esther anatarajia kwamba kwa kushinda tuzo, wanawake wengine watapata kuhamasika na pia kupata msukumo. Wanawake wanapaswa kujiwasilisha kote kote na kuleta mabadiliko duniani. Dhima ya uanauchumi ni kusaidia kubadilisha ulimwengu uwe bora zaidi. Wito wa Esther kwa wanawake wengine ni kujitoma katika uwanja wa uanauchumi ili kuboresha hali ya maisha katika dunia.

poverty economics africa
Good Economics for Hard Times ni kitabu kilichoandikwa na Abhijit V. Banerjee na Esther Duflo.

Hitimisho

Esther Duflo amechangia moja kwa moja na vinginevyo katika sera za kitaifa na kimataifa. Michango yake kutokana na mbinu ya kimajaribio kujaribu kutatua matatizo imehamasisha mashirika yote—ya kibinafsi na ya umma— kutathmini mipango yao ili kupambana na umaskini kwa ufanisi.

This post is also available in en_US.