Afrika ni bara lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi kutokana na hali yake nzuri ya anga kwa kilimo, wingi wa maliasili, wanyamapori, sera bora za uchumi na kadhalika. Bila shaka, ni sehemu bora kwa ajili ya uwekezaji. Hata hivyo, inaweza kuwa changamoto kulielewa soko la Afrika. Makala haya yatakusaidia kulielewa soko la Afrika pamoja na kukupa taarifa kuhusu baadhi ya biashara unazoweza kufikiria kuwekeza.
Aina za Biashara na Mawazo ya Faida ya Kibiashara Barani Afrika
1. Kilimo
Kutokana na hali nzuri ya hewa na mvua ya kutosha, Afrika ni eneo zuri la kufanya biashara ya mazao. Afrika inajulikana kwa kuyauza nje mazao ya kilimo kama vile kakao, kahawa na chai. Unaweza kuwekeza katika ufugaji wa kuku na kuyauza mayai mataifa ya nje au kuuza ndani mwa nchi. Pia, unaweza kuwekeza katika biashara ya maziwa au nyama. Ukiwa na kituo cha kusindika maziwa itakuwa na faida kwani utakuwa na bidhaa za maziwa zenye ongezeko la thamani kama vile mgando na jibini. Kilimo kina soko la tayari na hali ya hewa katika Afrika ni nzuri. Biashara hii inafaa katika nchi zenye hali nzuri ya hewa ya kilimo kama vile Uganda, Tanzania, Ethiopia na Tunisia.
2. Uagizaji Bidhaa na Huduma za Usafirishaji
Afrika haina huduma za kuaminika za uagizaji na usafirishaji. Kampuni nyingi za uagizaji bidhaa na huduma za usafirishaji zinamilikiwa na wawekezaji walioko nje ya Afrika. Hali hii inaibua fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa ndani wenye nia ya kujiingiza kwenye aina hii ya biashara. Sekta hii inatoa nafasi ambapo mwekezaji atahitajika kuliziba pengo hili kwa kutoa bidhaa na huduma zinazostahili.
Baadhi ya wateja katika biashara hii ni pamoja na taasisi za kiserikali za nchi za Afrika pamoja na mashirika yatakayohitaji huduma hizi. Ili uwe na mafanikio katika biashara hii, unahitaji mtandao mpana (wa wateja na usambazaji) na pia uwe na ubunifu. Baadhi ya nchi ambazo unaweza kuanzisha biashara hii ni pamoja na Rwanda, Botswana, Kenya, Congo na Ghana.
3. Biashara za Mtandaoni
Kutoa huduma za kibiashara kwenye mtandao ni mojawapo wa njia za kutarazaki barani Afrika. Changamoto kubwa ni ulaghai na utapeli. Hivyo basi, ili uwe mwenye mafanikio katika biashara hii, unahitaji kuwa na njia za kuondoa udanganyifu. Mazingira ya kirafiki kwa wateja na matangazo ya kutosha yanahitajika kwa ajili ya biashara hii. Kuna uchache wa kampuni za biashara ya mtandaoni barani na hii hujenga nafasi zaidi kwa wawekezaji wapya. Unaweza kuanzisha biashara hii Misri, Ethiopia, Rwanda, Kenya, Zimbabwe na Nigeria.
4. Ushauri wa kifedha
Afrika ina wajasiriamali wengi wenye ubunifu na vipaji na nafasi za biashara zinajitokeza kila siku. Kutona na wingi huu wa wajasiriamali, ipo haja ya ushauri wa kifedha ambapo wawekezaji wapya wanaweza kujifunza njia mbalimbali za kuwekeza fedha zao. Siri kwa aina hii ya biashara ni kuwa mwaminifu kwa wateja wako. Awali, wawekezaji wamekuwa wakitapeliwa na kupoteza fedha zao, na huwasababisha wawekezaji wengi kutotafuta huduma ya washauri wa fedha. Aina hii ya biashara inaafiki nchi za Afrika zenye uchumi imara kama vile Afrika Kusini, Misri, Kenya na Nigeria.
5. Kutoa Mtaji kwa Biashara Chipuzi
Afrika ina wajasiriamali wengi wenye ubunifu na vipaji, na nia ya kuanzisha biashara ila hawana mtaji wa kuanzisha. Kutoa mitaji kwa biashara chipuzi kwa wajasiriamali wa Afrika ni wazo bora lenye soko lililo tayari. Benki za Afrika hutoza viwango vya juu vya riba kwa mikopo ya kipindi kifupi na hivyo kukatisha tamaa wajasiriamali kukopa fedha. Yote unayohitaji kufanya ni kulielewa soko na hatimaye kuibua mahitaji ya soko hilo. Hata hivyo, biashara hii ina hatari ya juu ya hasara na hivyo utahitaji kuwa na njia za kuhakikisha kuwa mikopo kwa biashara chipuzi kwa wateja wako inatumika kwa madhumuni yaliyonuiwa. Pia, unahitaji kuwasiliana na mashirika ya udhibiti wa mikopo ili kuhakikisha usalama wa pesa zako.
6. Utayarishaji wa Filamu na Video
Afrika ina waigizaji wenye vipaji na ubunifu kwani idadi kubwa ya watu ni vijana, na hivyo basi watazamaji ni wengi. Ili uweze kujitosa kwenye biashara hii, unahitajika kutayarisha filamu na picha zenye ubora wa juu. Waigizaji wengi wa Afrika husafiri barani kutafuta huduma za hali ya juu. Kanda za filamu zinazotayarishiwa Afrika zimepata kutambuliwa pakubwa duniani. Baadhi ya nchi za Afrika ambapo filamu na biashara ya utayarishaji ina soko lililo tayari ni pamoja na Nigeria, Ghana na Tanzania.
7. Ununuzi na Uuzaji wa Ardhi na Majumba
Uhitaji wa ardhi kwenye maeneo yaliyokaribia majiji na miji umeshamiri Afrika. Kumiliki kipande cha ardhi ni mojawapo wa njia bora zaidi ya uwekezaji. Wafanyakazi wengi wapya hulipa kipaumbele suala hili kwa kununua kipande kikubwa cha ardhi na kisha kugawanya kuwa vipande vidogo na kuviuza kwa faida kubwa. Hii ni njia itakayokuhakikishia faida kutokana na mauzo. Isitoshe, thamani ya ardhi hupanda kutokana na ongezeko la mahitaji kila siku. Nchini Kenya na Tanzania, kwa mfano, biashara hizi zimefana sana.
8. Huduma za Usafiri (Teksi)
Hili ni wazo zuri la biashara hasa katika miji mikubwa ya Afrika. Idadi kubwa ya watu wenye kipato cha juu wanapendelea huduma za teksi kwa safari zao ndefu au hata za muda mfupi. Vilevile, baadhi ya kampuni hukodisha huduma za teksi kwa baadhi ya wasimamizi wao wakuu, badala ya kuwapa magari. Unaweza kupata huduma hii ukiwa barabarani au uagize teksi kwa kutumia simu. Ili kufanikiwa katika biashara hii, unapaswa kuhakikisha kiwango cha juu cha usalama wa gari, pamoja na kuwachukua wateja kwa wakati unaotakiwa. Biashara hii inafaa hasa kwa uchukuzi wa majiji na miji.
9. Maandalizi ya Sherehe na Matukio
Kila siku, Waafrika wanajihusisha na sherehe ya kila aina. Hata hivyo, kupanga na kuandaa sherehe huwa kero hasa kukusanya rasilimali zinazohitajika na kwa watu waliolengwa. Mara nyingi, hapana utaratibu wa mipangilio ya sherehe na matukio na hivyo basi ipo haja ya kuwepo kwa huduma za kuhakikisha mipango na maandalizi kabambe yamefanywa bila tatizo kwa wenye sherehe au tukio hilo.
10. Mafunzo Kwa Wafanyakazi
Ongezeko la mahitaji ya mafunzo kwa wafanyakazi katika sekta ya ajira ni kubwa mno. Wengi wa wahitimu kutoka vyuo vikuu vya Afrika wanahitaji kozi nyingine ya kujiandaa kwa ajili ya ajira. Hali hii inaleta haja ya kuwepo kwa taasisi zaidi za mafunzo ya kitaalamu. Baadhi ya maeneo unayoweza kutoa mafunzo ni pamoja na uendeshaji wa shughuli za kiofisi na jinsi ya kutumia fedha vyema. Wazo hili la kibiashara ni zuri katika nchi za Afrika zenye mifumo imara ya elimu kama vile Nigeria, Afrika Kusini na Kenya.