Silicon Savannah: Jinsi Vitovu vya Kiteknolojia Vinachangia Kukuza Uchumi

Tafsiri:
No available translations found

Nairobi imekuwa chimbuko la uvumbuzi nchini Kenya, na huku kumechangia sana kuongezeka kwa mazingira ya kiteknolojia maarufu kama ‘Silicon Savannah.’ Mazingira haya ya kiteknolojia yamegeuza Nairobi kuwa sehemu ya kipekee kwa wawekezaji na wapenzi wa teknolojia. Uvumbuzi muhimu nchini Kenya siku hizi unaweza kupatikana kupitia vituo hivi vinavyokuza na kuchapuza uvumbuzi huu.

tech hub kenya
Sote ni kitovu cha teknolojia huko Voi, Kenya.

Kenya inashuhudia ukuaji wa kiuchumi hasa kutokana na kitovu cha teknolojia cha iHub kilichoanzishwa mwaka 2010. Tangu wakati huo, vitovu vya kiteknolojia vimechipua kwa kiwango kikubwa katika miji mikubwa nchini Kenya. Baadhi ya vitovu hivi vya kiteknolojia ni pamoja Swahilibox huko Mombasa, Lakehub mjini Kisumu, Dlab Hub mjini Eldoret, Sote Hub kule Voi, Ubunifu mjini Machakos na Mount Kenya Hub mjini Nyeri.

Vitovu hivi vya kiteknolojia vinafanya kazi kwa kutegemeana huku vingine vikifanya kazi kwa kushirikiana na taasisi za elimu. Muhimu zaidi ni kwamba vyote vinalenga kusaidia wajasiriamali katika sekta ya teknolojia, ubunifu na utamaduni.

Kusogeza kwa Vitovu vya Teknololojia kwa Miji Midogo

Kutokana na kujaliwa kwake kwa utajiri wa kirasilimali, mji mkuu Nairobi umeishia kwa mshali faafu kwa biashara nchini Kenya. Hata hivyo, umeishia kuwa mji ghali kwa vijana kuishi na kufanya biashara kwani takribani kila soko limejaa. Ili kufanya vitovu vya kiteknolojia kuwafikia watu wengi zaidi, imeonekana kuwa heri kuhamia katika miji na maeneo mengineyo. Moja ya vitovu vilivyoondoka Nairobi hivi karibuni ni SwahiliBox iliyohamia Mombasa.

Kitovu cha Makers nchini Kenya kilichoundwa kutoa huduma kwa vijana wenye kipato cha chini ili wajiwezeshe kielimu na kiteknolojia.

Jinsi Vitovu vya Kiteknolojia Vinachangia Kukuza Uchumi

Ustawi, uvumbuzi na ukuaji ni vipengele muhimu linapokuja suala la kuamua ukuaji wa uchumi. Hii ni kwa sababu wawekezaji huzingatia mambo haya ili kuamua ambapo wanaweza kuwekeza. Kwa hiyo, vitovu vya kiteknolojia huwa na nafasi muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Kenya. Zifuatazo ni njia ambazo vitovu hivi vya kiteknolojia huchangia ukuaji wa uchumi.

1. Kuibua Nafasi za Kazi za Moja kwa Moja

Sekta ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano ina jukumu muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchini. Vitovu vya kiteknolojia huibua ajira nchini Kenya kupitia mabadiliko na mageuzi ya sekta vya kiteknolojia, na hivyo kuwaajiri maelfu ya vijana.

Sekta hii pia inachangia kupanuka kwa bidhaa na huduma, na hivyo kupanua masoko. Hali hii hukuza ujasiriamali na wananchi wanaweza kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa. Pia, serikali ya Kenya inaweza kupanua vyanzo vya mapato kutokana na kodi inayoweza kuimarisha sekta ya elimu, huduma za afya na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

2. Kuibuka Kwa Huduma Na Ujenzi Wa Viwanda

Vitovu vya kiteknolojia nchini Kenya vimeelekea kupanua huduma na sekta mbalimbali. Hii ni hasa kutokana na uvumbuzi unaosababisha kuanzishwa kwa huduma kupitia simu za mkononi kama M-Pesa na huduma za hifadhi ya kimawingu. Teknolojia, Habari na Mawasiliano imesababisha kuibuka kwa sekta ya kuunda programu (apps). Kwa mfano, Facebook imechangia ajira kwa vijana wengi huku ikiendeleza biashara ya matangazo. Watu wengi wanapoajiriwa na huduma kuongezeka, mapato zaidi yanazalishwa.

3. Uvumbuzi katika Biashara

Zaidi ya asilimia 95 ya biashara zenye mafanikio hufanya matangazo yake mitandaoni. Mtandao hutoa njia ya kuwafikia wateja na hivyo kuchangia kupata soko. Mitandao ya kijamii ni mojawapo ya njia zinazoongoza katika matangazo nchini Kenya kwani inaweza kufikia soko (wateja) pana. Mitandao ya kijamii husaidia biashara kubuni njia mpya za kufanya biashara, na hivyo kuboresha ufanisi.

4. Kubadilisha Mifumo ya Wafanyakazi

Kampuni za kimtandaoni kama vile Upwork zimebuni ajira mtandaoni kwa vijana wa Kenya. Kutokana na idadi kubwa ya vijana wasio na ajira nchini Kenya, kuchukua majukumu na kazi ambazo ni zinatekelezwa kupitia mtandao kumesaidia kubuni ajira kwa maelfu ya vijana. Kwa hiyo, vitovu vya kiteknolojia vimeleta mageuzi ya mifumo ya wafanyakazi na kusaidi kusogeza kazi kutoka nchi moja hadi nyingine. Ajira hizi huwawezesha Wakenya kubadilisha uchumi kwani wananchi wanaweza kujifanyia kazi wenyewe.

5. Kuchangia kwa Ukuaji katika Pato la Taifa

Vitovu vya kiteknolojia vinachangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa la Kenya. Kutokana na uvumbuzi, watu wanauza mawazo yao kwa mataifa mengine na hivyo kujichumia mapato. Nchini Kenya, kampuni nyingi zinazoendesha biashara mtandaoni zimejitokeza kutokana na vitovu hivi vya kiteknolojia. Kampuni hizi hutegemea utandawazi ambao huchangia katika ukuaji wa Pato la Taifa. Pamoja na mahitaji makubwa ya biashara ya mtandaoni kutokana na intaneti ili kutimiza biashara za mitandaoni, Kenya ipo katika harakati za kuwa miongoni mwa nchi zilizoendelea. Pia, kuendelea kwa teknolojia kunasababisha uvumbuzi wa njia tofauti za kuendesha biashara, hivyo basi kukuza wajasiriamali.

Silicon Savannah na Mustakabali wa Teknolojia, Habari na Mawasiliano wa Kenya

Ni bayana kuwa vitovu vya kiteknolojia vinastahili kuhimizwa na Serikali ya Kenya inapaswa kuendelea kuwekeza sana katika shughuli za vitovu hivi. Hii ni kutokana na kwamba vitovu hivi huchangia kuwakuza wataalamu katika nyanja za Teknolojia, Habari na Mawasiliano na ujasiriamali. Isitoshe, taasisi za elimu ya juu lazima ziwekeze katika vitovu vya kiteknolojia ili kukuza mawazo zaidi na uvumbuzi.