Je, unatafuta biashara unayoweza kuianzisha nchini Kenya ukiwa na mtaji mdogo? Makala hii itakuonyesha biashara 6 ambazo unaweza kuanzisha mara moja kwa mtaji mdogo. Labda una wazo la kibiashara na unadhani kuwa huwezi kuanzisha kwa sababu huna mtaji wa kutosha. Unaweza kuanza biashara ukiwa hata na shilingi 1,000 na kuikuza. Unahitaji tu kufanya kazi kwa bidii, ukakamavu, na kujiamani. Yafuatayo ni baadhi ya mawazo ya kibiashara kwa watu wenye kipato cha chini nchini Kenya.
Soma makala hii kwa Kiingereza: 6 Businesses You Can Start With Little Capital in Kenya
Biashara ya mtaji mdogo Tanzania: Ingawa makala hii iliandikwa kwa ajili ya wasomaji wa Kenya, biashara zilizoorodheshwa hapa pia ni biashara za mtaji mdogo zenye faida kubwa Tanzania. Hivyo kama wewe uko Tanzania, endelea kusoma makala hii itakusaidia.
Jinsi ya Kuanza Biashara na Mtaji Mdogo
Kuwa na mtaji mdogo sio sababu ya kukuzuia kuanzisha biashara yako na kukuza kipato chako polepole. Kama una mawazo ya biashara kwa mtaji mdogo, kati ya mambo ya kuzingatia wakati wa kuanza ni:
- Haijalishi mtaji wako ni mdogo kiasi gani, anza kidogo tu
- Fanya utafiti kamili kuhakikisha kuwa umechagua eneo bora kwa biashara yako
- Anzisha biashara inayohusisha mambo unayoyafahamu ili usipoteze muda na fedha ukijifunza mambo mapya.
- Ikiwa mtaji wako hautoshi, unaweza kushirikiana na rafiki yako au jamaa
- Kwa kuwa huitaji mtaji mkubwa kuanza, unaweza kuomba mkopo au msaada wa fedha kutoka kwa wapendwa wako
- Jaribu kubadilishana mawazo na watu ambao wamekomaa kwenye biashara unayotaka kuanzisha
- Tangaza biashara yako kwa kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook bila gharama kubwa ya matangazo
Biashara ya Mtaji Mdogo 2021
1. Biashara ya Mitumba
Hii ni biashara ya mtaji mdogo unayoweza kuanza hata kwa shilingi 1,000. Biashara hii ni faafu katika maeneo ya mijini. Vijana wengi wamewekeza katika biashara hii na wanaishia kufanikiwa. Wengi wao hununua nguo za mitumba kutoka Muthurwa na soko la Gikomba ambapo bei huwa ni nafuu. Kwa bahati nzuri, huhitajiki kwa na duka. Unahitaji tu kuzitandaza nguo zako kwenye gunia.
Pia, unaweza kuuza nguo za mitumba kwa wafanyakazi wenzako na marafiki. Unachohitaji ni kujua aina ya mavazi wanayopenda wateja wako wa mara kwa mara, na kisha uwafikishie. Baada ya kipindi fulani, utakuwa umechuma mtaji wa kutosha kwa minajili ya kupanua biashara yako na hata kufungua duka katika eneo zuri.
2. Kuuza Mikoba ya Wanawake
Hii ni biashara ambayo imeshamiri kwani wanawake wengi wanaipenda mitindo sana. Unaweza kuanza kuiuza mikoba kwa kuanza na mkoba mmoja tu. Unaweza kununua mikoba hii kwa bei ya chini mtaani Eastleigh. Sio lazima ununue mikoba mipya, unaweza kuanza kwa kununua toka kwa wale wanaofanya biashara ya mikoba ya mitumba. Iwapo una kurasa za mitandao ya kijamii kama Facebook au Instagram, unaweza kuwa ukipachika picha na hivyo kujihakikishia maozo kutokana na wafuasi wako. Hii ni biashara ambayo unaweza kufanya hata kama umeajiriwa. Unahitjika tu kubeba mikoba michache kwenda nayo kazini na unaweza kuwauzia wafanyakazi wenzako.
3. Kuuza Matunda na Maji ya Matunda
Hii ni njia nyingine yeneye faida kubwa ya biashara ambayo unaweza kuanza kwa chini ya shilingi 3,000. Unahitaji tu kuwa na mashine ya kusaga na kuchanganya matunda, na matunda kwa wingi. Ili kupunguza gharama yako hata zaidi, unaweza kupanda mwenyewe baadhi ya matunda. Huhitajiki kuwa na shamba ili kuanza. Unaweza kutafuta magunia machache na kuyajaza udongo. Kisha, panda matunda kama vile karakara na tikiti maji. Unaweza pia kuongeza mboga nyingine kama vile giligilani na kabichi. Mboga hizi zinaweza kuleta mapato ya ziada, hasa ikiwa unauza katika maeneo ya mijini.
4. Kuuza Mayai
Hii ni moja ya biashara za mtaani maarufu. Unaweza kuanza kuuza mayai kwa mtaji wa shilingi 1,000. Hii ni biashara ambayo haihitaji muda wako mwingi. Unaweza kuanza kwa kununua jimbi wa kienyeji mmoja. Hii itakugharimu takriban shilingi 500. Kisha, unaweza kununua jogoo kwa shilingi 800 na utakuwa tayari kuanza biashara hii. Subiri kuku waanze kutaga mayai na kisha unaweza kuanza kuyauza. Kuku wa asili (kienyeji) ni bora kuwa wanaweza kujitafutia chakula chao wenyewe. Unahitaji kuwaachilia huria wakati wa asubuhi na kuwafunga jioni. Hii inarahisisha gharama ya kuwafuga. Hata hivyo, unahitaji kutenga mahali maalum ambapo wanaweza kuyataga mayai. Vilevile, ni vyema ukitenga baadhi ya mayai ambayo yanaweza kuanguliwa vifaranga. Utashuhudia biashara yako ikikua bila mchango wa ziada.
5. Kuuza Maziwa
Biashara ya kuuza maziwa ni moja ya biashara za mtaji mdogo. Watu wengi katika maeneo ya mijini wanayategemea maziwa yaliyofungwa. Hata hivyo, wapo wengi ambao wangetaka kutumia maziwa mabichi. Hii inaibua wazo la kibishiara lenye faida kubwa ambayo unaweza kufikiria kuwekeza. Aidha, unaweza kuuza maziwa pamoja vitafunio kama vile keki. Ili kuongeza mapato yako, unaweza kupata mafunzo ya jinsi ya kutengeneza mtindi. Unaweza kuwa ukiwapelekea watu mtindi na vitafunio katika ofisi zao. Ili kuimarisha mauzo, unahakikisha ya kwamba umefungua duka lako katika eneo lenye shughuli nyingi au karibu na hospitali au shule.
6. Kuuza Chakula Katika Maeneo ya Ujenzi
Ni bayana kuwa hii ni biashara ambayo una uhakika wa faida. Kile unahitaji kufanya ni kuandaa vyakula na kupeleka katika maeneo ya ujenzi. Kuna miradi mingi inayoendelea ya mali isiyohamishika nchini ili kukidhi idadi ya Wakenya inayokua. Miongoni mwa vyakula mwafaka katika maeneo haya ya ujenzi ni pamoja na githeri na ugali. Mbali na hilo, unaweza kuyaongeza mapato yako kwa kuuza uji. Biashara hii inahitaji mtaji wa shilingi 2,000.