Tambua Ulaghai wa Bitcoin (Bitcoin Scam)

Tafsiri:
en_US

Bitcoin na sarafu nyinginezo za kidijitali zinazidi kukubalika katika nchi za Afrika kama vile Botswana. Hata hivyo, pana ukosefu wa elimu ya jumla na ufahamu kuhusu sarafu hizi na jambo hili limesababisha ongezeko la visa vya ulaghai vya Bitcoin vinavyolenga Waafrika.

Bitcoin ni mfumo unaojitegemea wa sarafu za kidijitali bila benki kuu au msimamizi mmoja ambao anaweza kuwaunganisha watumiaji mtandaoni.

Kiotomotela cha Bitcoin nchini Botswana ni moja ya viotomotela vya Bitcoin 10 barani Afrika.

Bitcoin imekuwa na misukosuko tangu kuanzishwa kwake. Bei yake ni mojawapo ya mambo ambayo huvutia watu wengi. Bitcoin si imara sana, kwa kuwa bei yake inaweza kwenda juu na chini sana katika vipindi vya muda mfupi. Hata hivyo, kwa muda mrefu sasa, bei imeelekea hasa kwenda juu.

Bitcoin ni njia bora sana ya kuhifadhi fedha kwa muda mrefu, sawia na akaunti ya benki. Mbali na kuwa huria, bila yeyote wa kudhibiti ina maana kwamba ugavi ni mdogo. Kutakuwa tu na Bitcoin milioni 21 milele. Uzuri wake ni kuwa Bitcoin 1 imegawanywa katika satoshi milioni 100 na hivyo huna haja ya kununua Bitcoin nzima. Mwaka wa 2019 dhana ya “stacking sats” ilikuwa stihizai (meme) maarufu mtandaoni.

Ulaghai wa Cryptocurrency

Baadhi ya visa vya ulaghai wa hali ya juu barani Afrika ni pamoja na:

  • Kampuni ya uwekezaji ya Bitcoin, Velox 10, ilitoweka na mamilioni ya shilingi za Kenya katika 2019.
  • Kampuni ya Bitcoin, Calabar, ilitoweka na mamilioni ya naira za Nigeria. Kampuni hii ilikuwa imewaahidi wateja asilimia 30 ya mapato kutokana na biashara ya mtandaoni ya Bitcoin.
  • Mwezi Mei 2018, taasisi za kiserikali za Afrika Kusini zilisema kuwa walikuwa wakichunguza madai ya ulaghai wa Bitcoin, ulioshirikisha kampuni inayoitwa Bitcoin Global iliyowatapeli wawekezaji randi bilioni 1 (milioni 80 za Kimarekani) kwa ahadi ya kuwapa mavuno makubwa. Kampuni hii iliahidi wateja kwamba wangeweza kupata asilimia 2 kwa siku, asilimia 14 kwa wiki na asilimia 50 kwa mwezi.
  • Waafrika Kusini wenye hamaki walivamia, wakapora na kuchoma moto nyumba ya mtu ambaye aliripotiwa kuendesha biashara laghai ya Bitcoin nchini Afrika Kusini.

Ishara za Ulaghai wa bitcoin

Tumeweza kuandaa muhtasari wa ishara za maonyo dhidi ya ulaghai wa Bitcoin.

Mpango wa Ponzi wa Bitcoin

Mpango wa Ponzi ni aina ya utapeli unaowavutia wawekezaji kwa kuwalipa faida wawekezaji wa awali (watangulizi) kwa kutumia fedha kutoka kwa wawekezaji wengine wageni (wapya). Maelfu ya Waafrika Kusini walipoteza fedha zao mwaka huu kutokana na mpango wa ponzi, ambayo uliwaahidi faida ya asilimia 100 kwa siku 15.

Tovuti za Hadaa

Hadaa za aina hii hutokea kama jaribio la ulaghai wa kupata taarifa nyeti kama vile majina ya watumiaji, nywila na maelezo ya kadi za benki. Katika hali hii, tovuti huhadaa watumizi wa Bitcoin kubainisha ufunguo wa kipekee wa Bitcoin. Ufunguo wa kipekee huhusisha nambari ya siri ambayo hutumika kwa kupokea au kutuma Bitcoins zako kwa anwani nyingine ya mtumiaji wa Bitcoin.

Toleo la Awali Bandia (ICOs)

Unahitaji kuwa mwangalifu na kuchukua muda wa kukusanya taarifa zaidi kuhusu ICOs mpya zinazotoa ahadi za mapato makubwa nay a haraka.

Kumbuka kuwa tunaamini kwamba ICOs “halisi” mara nyingi huhusisha ulaghai mwingi hivyo hupaswi kuekeza. Jambo la busara la kufanya ni kuhifadhi Bitcoin kwa muda mrefu kwani pana uwezekano wa kukupa faida nzuri. Hapana haja ya kuparamia mapato hata ya juu zaidi.

Ada ya Uanachama au Mafunzo

Mojawapo ya dalili za ulaghai wa Bitcoin ni wakati unashawishiwa kulipa ada kwa ajili ya uanachama au kupata mafunzo ya Bitcoin na Bitcoin mbadala.

Mkoba Bandia

Mkoba wa sarafu za kidijitali ni mkoba salama ambao hutumika kuhifadhi, kutuma, na kupokea fedha za kidijitali kama Bitcoin. Unahitaji kuwauliza watumiaji wenye uzoefu wa sarafu za kidijitali kuhusu mkoba maalum ambao unakusudia kutumia au kusoma maoni yanayohusu mkoba huo kwenye tovuti za kuaminika.

Uchimbaji Mawinguni (Cloud Mining)

Bitcoins husanidiwa kwa njia ya “uchimbaji”. Hii ni mbinu yenye gharama kubwa kwa mujibu wa vifaa na wakati. Hata hivyo, kwa kutumia teknolojia ya uchimbaji mawinguni una uwezo kuchimba bila kuhitaji vifaa kwa kutumia huduma za uchimbaji mawinguni kwa ada. Kuna huduma za kihalali za uchimbaji ila unahitaji kuwa makini zaidi wakati wa kuchagua huduma maalum utakayotumia.

Kwa ujumla, kama unataka faida ya Bitcoin, unahitajika kujua vizuri sana unachokifanya. Baadhi ya mbinu za uchimbaji wa mawinguni hazina faida, hata kama si njia za ulaghai.

Tunu za bure

Baadhi ya matapeli hutoa tunu za bure za Bitcoin na kuwataka watu kutuma fedha, Bitcoin au maelezo ya kibinafsi kwa ajili ya usajili. Aghalabu, tunu hizi huwa zimesheheni ulaghai.

Mbinu Nyinginezo Zisizo za Utapeli wa Moja kwa Moja

Mabadilishano ya Fedha
Soko la mabadilishano huhusisha soko la kidijitali ambapo watu wanaweza kununua na kuuza Bitcoins. Kwa mfano, watu wengi walikuwa wamenunua Bitcoin zao za kwanza kutoka Mt. Gox na kuziacha Bitcoin kwenye soko hilo. Mt. Gox ilifunga shughuli zake za kibiashara na miaka mingi baadaye, bado haijajulikana jinsi watu wanaweza kupata tena fedha zao walizokuwa wameekeza.

Kwa ujumla tunaweza kusema: Bitcoin si zako iwapo huna funguo za waleti yake.

Unatakiwa kuhifadhi Bitcoin kwenye simu yako, mkoba wa karatasi au mkoba wa kifaa kwani ni wajibu wako; kwa ajili ya usalama wako mwenyewe na nakala ya hifadhi zako.

Kwenye soko la mabadilishano ya fedha, unaweza pia kupata kujaribiwa kujiingiza katika biashara ya Bitcoin mbadala (altcoins).

Altcoins

Bitcoin mbadala (Altcoin) ni aina yoyote ya sarafu za kidijitali isiyo Bitcoin. Bitcoin mbadala nyingi pengine huanzishwa na watu wenye nia nzuri, lakini hatimaye, tafakari haya:

  • Kila mmoja wa wanzilishi wa Bitcoin mbadala watahifadhi sehemu kubwa ya utajiri wao kwenye Bitcoin.
  • Kama kitu chochote kibaya kitawatokea waanzilishi wa Bitcoin mbadala, bei yake ina uwezekano wa kuanguka kwa kasi.
  • Hakuna Bitcoin mbadala yenye kiwango chochote cha usaidizi, usalama, programu zinazopatikana, matumizi yanayofahamika sana kama Bitcoin.

    Ni bora kuepuka biashara ya aina yoyote ya Bitcoin mbadala. Ni kama michezo ya kamari, pengine unaweza kupata pesa kama wewe una bahati. Hata hivyo, unaweza ukafikiri kuwa wewe una uelewa na kuishia kutumia muda mwingi katika kamari (bahati nasibu) na mwishowe utadhurika usipate faida kama ilivyofanikishwa na Bitcoin.

Vidokezo vya Usalama

1. Fanya utafiti wa mwanzilishi au wanzilishi wa kampuni za Bitcoin kwa ajili ya kumbukumbu za uhalifu au shughuli zozote za biashara zisizoaminika.

2. Hifadhi fedha katika programu za mkoba.

3. Hifadhi mkoba wako kwa kutumia msimbo.

4. Mkoba wa kifaa ni mojawapo ya chaguzi salama kwa ajili ya kuhifadhi Bitcoin.

Mkoba wa Bitcoin wa kifaa.

5. Kuwa na pochi mbalimbali.

6. Weka salama nakala ya pochi yako.

7. Tumia hatua mabili za uthibitisho.

8. Kamwe usitambulishe nambari za siri kwa mtu yeyote.

9. Pakua mkoba wako kutoka maduka ya program yaliyothibitishwa.

10. Kama umeathirika, ripoti tatizo kwa polisi na uwatahadhari marafiki zako wote, wafanyakazi wenza na familia ili kuwalinda.

Marafiki na familia

Bitcoin ni teknolojia ya kusisimua, hivyo ni jambo la kawaida kutaka kushirikisha watu unaowajali. Ni vizuri kutoruhusu kutawaliwa na teknolojia hii. Ikiwa wewe mwenyewe unashikilia thamani ya teknolojia hii, ina maana kwamba mtu mwingine anaweza kufuatilia kwa urahisi kutoka kwako.

Kama kuna yeyote anayejua kushiriki kwako kwa Bitcoin, hii inaweza kuwa hatari kwa usalama baadaye. Kama bei itaenda juu, kama ilivyokuwa katika siku za nyuma, ukimiliki Bitcoin yenye thamani ya dola 100, unaweza kununua nyumba ukitumia fedha hizo katika kipindi cha miaka 10. Hivyo basi unahitaji kuwa na maisha ya hadhi ya chini (kwa mfano usinunue magari ya kifahari) na kamwe usitambulishe kiasi gani cha Bitcoin unachomiliki. Mtu anapouliza kiwango unachomiliki, “Kiasi cha haja” ni jibu mwafaka.

Hitimisho

Pindi tu baada ya kupoteza fedha katika ulaghai wa Bitcoin, haiwezekani kuzipata tena. Shughuli na biashara za Bitcoin hazidhibitiwi na benki kuu au mashirika yoyote ya kifedha ya kiserikali. Aidha, mabadilisho ya Bitcoin hayawezi kugeuzwa. Ni kwa sababu hii, unahitajika kuchukua tahadhari ya ziada wakati wa kushughulika na Bitcoin.

Soma Zaidi