Kampuni Chipuzi za Bima Zinazotoa Huduma ya Afya kwa Wananchi wenye Mapato ya Chini Nchini Kenya na Tanzania

Tafsiri:
en_US

Kampuni za bima hutoa huduma mbalimbali kwa lengo la kupunguza hasara za kifedha zinazoweza kutokana na majanga ya kiafya yasiyotarajiwa. Hata hivyo, kupokelewa kwa huduma hizi bado ni kwa kiasi cha chini kabisa barani Afrika. Kwa mfano, nchini Kenya na Tanzania, kupenyeza kwa bima ni kwa asilimia 2.9 na 0.7 mtawalia. Takwimu hizi za chini hasa zinatokana na sababu kuwa kampuni za bima kwa kawaida zimekuwa zikitumia mfumo sawia na wa mataifa yaliyoendelea kinyume na kujenga bidhaa ambazo zinakidhi mahitaji ya wenyeji.

Tanzania na Kenya hazina huduma za afya ya bure kwa wote.

insurtech tanzania
Jamii Africa ni bima ndogo tamba ya afya kwa sekta isiyo rasmi nchini Tanzania.

Kampuni hizi za bima “Insurtech” zinahususisha matumizi ya uvumbuzi wa teknolojia iliyoundwa ili kuimarisha akiba na ufanisi kutokana na mfumo wa sasa wa sekta ya bima. Insurtech ni mseto wa maneno “insurance” na “technology,” kutokana na jina lenye muundo sawia fintech. – Investopedia

Kampuni za bima ya kiteknolojia zinanuia kubadilisha mtindo kwa kuwezesha bidhaa zinazokidhi mahitaji mahsusi ya wateja. Taasisi hizo hutegemea teknolojia, utafiti, na ubunifu ili kupata data muhimu kuhusu tabia ya fedha na mahitaji ya wateja wao walengwa. Matumizi bora ya teknolojia ya akili bandia yamewezesha kampuni za bima mbalimbali kutoa bidhaa ambazo ni nzuri kwa ajili ya kundi fulani la watu.

Katika makala haya, mkazo upo kwenye kampuni chipuzi za bima ya kiteknolojia zinazolenga wananchi wa kipato cha chini nchini Kenya na Tanzania. Hizi kampuni ndogo za bima ya kidijitali zinanuia kulinda wateja wao kutoka kuzama zaidi katika umaskini kwa kuwaandalia sera za bima nafuu na zinazopatikana.

 

Turaco (Kenya)

Shughuli za Turaco zina msingi wake katika hoja kwamba asilimia 90 ya Waafrika hawana bima ya afya ilhali watu milioni 89 katika eneo hili wanakabiliwa na matatizo ya afya kila mwaka. Hivyo basi, wanakusudia kutoa bidhaa ambazo zitawaruhusu wateja wake wajipatie huduma bora za afya ikilinganishwa na fedha wanazochuma.

Kampunu hii, ambayo ilianza kazi mwaka 2018, kwa sasa inatoa huduma zake Uganda na Kenya ingawa ina lengo la kuingia katika masoko mengine ya Afrika katika siku za karibuni. Kwa kushirikiana na wakopeshaji fedha kwa njia ya simu na kampuni nyingine, Turaco imeweza kutoa huduma kwa watu waliotelekezwa na wasionufaika na sera nafuu na kupatikana kwa bima ya maisha na ya matibabu.

Insurtech startup in Kenya
Kampuni ya Bima ya Turaco.

Tangu kuanzishwa kwake, imeweza kutoa bima kwa zaidi ya watu 30,000 kutokana malipo yake ya chini ya kila mwezi ambayo huanzia shilingi 200 (dola 2). Hasa, imeweza kupata ruzuku ya fedha hivi karibuni ya ufadhili wa milioni dola 1.2. Kwa msaada huo wa fedha, inatarajia kufikia mamilioni ya watu hivi karibuni. Kutimiza kwa lengo hili kutakuwa na manufaa ya kuhakikisha kuwa Waafrika zaidi wanapata huduma za afya bora.

JamiiAfrica (Tanzania)

Ilianzishwa mwaka 2015 na imekuwa mojawapo ya kampuni chipuzi za bima ya kidijitali inayokua kwa kasi nchini Tanzania. Bidhaa yake kuu, Jamii, ni bima ya matibabu inayokidhi mahsusi wale walioko katika sekta zisizo rasmi. Bima hii tamba ya matibabu bima ilitokana kwa ushirikiano kati ya Jubilee Insurance Tanzania Limited, Edgepoint Digital Limited, na Vodacom Tanzania Limited.

 

Wateja walengwa ni Watanzania ambao mapato yao ni chini ya TZS 161,000 (dola 70) kwa mwezi. Kwa kuendesha shughuli za kiofisi kwa njia ya simu ya mtumiaji, Jamii Africa imeweza kupunguza gharama za kuhudumu kwa hadi asilimia 95. Kutokana na hili, bidhaa zake huanzia kama TZS 2300 (dola 1) kwa mwezi. Kampuni hii ina zaidi ya watumiaji 20,000 na inatambulika katika vituo vya afya zaidi ya 400.

Bluewave (Kenya)

Sawia na kampuni chipuzi za bima ya kidijitali zilizotajwa katika makala hii, Bluewave hunuia kuwezesha sera ya bima nafuu kwa watu wenye kipato cha chini. Kwa kupunguza gharama ya kampuni ya bima ya kushiriki, pana uwezo wa kupunguza malipo ya kila mwezi yanayolipwa na wateja. Mojawapo ya bidhaa zake muhimu ni Imarisha Jamii. Hii ni sera ya bima ya matibabu ambayo inalenga kuhudumia mahitaji ya matibabu ya wananchi wa kipato cha chini nchini Kenya. Shughuli hizi huendeshwa na Jubilee Insurance.

 

Katika mahojiano na East African Business Times Magazine, Mkurugenzi Mtendaji Adelaide Odhiambo alisema,

Imarisha Jamii amefungua fursa kwa mtu yeyote kati ya umri wa miaka 18 na 65 bila kujali hali yao ya awali ya kiafya kwa kukidhia gharama za hospitali, za ulemavu, na hata kifo kwa gharama ya shilingi. 20 kila wiki.

Watumiaji walio na aina yoyote ya simu ya mkononi wanaweza kupata bidhaa hii ya bima kwa kupiga *643# na kuchagua *Imarisha Jamii*. Baada ya haya, wanatakiwa kufuata maagizo yaliyowasilishwa. Mtu anaweza kufanya malipo ya kila mwezi au kila wiki kupitia M-Pesa.

World Cover (Kenya)

Kwa miaka mingi, kilimo kimekuwa kama uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya. Hakika, asilimia kubwa ya Wakenya hujishirikisha katika kilimo kidogo. Huku kazi hii ndiyo chanzo kikuu cha mapato kwa wengi wao, mazao mabaya ya msimu mmoja tu yanaweza kuwatia katika umaskini. Uhalisia huu unafanya kuwa muhimu kwa wakulima wadogo wadogo wa Kenya kupata bima inayowafaa. Kwa bahati mbaya, kampuni za kijadi mara nyingi hutoa chaguzi za bima ambazo ni zaidi ya uwezo wao wa kifedha. World Cover wameingia katika soko hili kwa ajili ya kutoa huduma mwafaka.

Insurtech startup in Kenya
World Cover Insurance.

Kampuni hii chipuzi ya bima, ambao ilianza kazi katika mwaka wa 2015, inatumia mipangilio ya kiteknolojia ambayo imekarabatiwa kwa usahihi ili kuangazia matukio yanayohusiana na mvua, kwa kuchunguza aina ya mimea na ukanda husika wa kilimo. Hii imewezesha utendekaji wa haraka na wa papo hapo ili kulipwa kwa madai ya wakulima kupitia mbinu za malipo ya pesa mkononi kama M-Pesa. Kwa mfano, mwezi Februari 2019, kampuni hii iliwafidia wakulima wa Kenya kupitia bima kutokana na mazao duni na kiangaza kilichoshuhudiwa nchini kote.

BIMA (Tanzania)

BIMA ni mojawapo ya kampuni chipuzi za bima za kidijitali ambazo zimeathiri familia nyingi Tanzania. Kwa mfano, BIMA Mkononi imebadilisha sekta ya afya nchini Tanzania. Kwa kuikumbatia teknolojia ya kisasa ya simu, kampuni hiyo imewezesha kuwepo kwa bima kii kwa watu ambao hapo awali waliona bima ya afya kuwa ya kifahari tu. BIMA, inayojulikana kama MILVIK, iliibua ushirikiano na watoa huduma za mawasiliano ya simu, Tigo, ili kuwaruhusu watu kupata huduma hii ya bima kwa njia ya Tigo Pesa. Resolution Insurance ndiyo kampuni ya bima inayotekeleza huduma hii.

 

Mtu anaweza kupata Bima Mkononi kutoka kiwango cha chini kama shilingi 2,999 (dola ​​1.31) kwa ajili ya bima ya miezi 2. Kwa kiasi hiki, mtu anaweza kudai hadi shilingi milioni 1.2 (dola 522.22) katika muda wa saa 72 baada ya kuwasilisha nyaraka zinazohitajika. Kwa vile BIMA ni huduma inayoendeshwa na teknolojia inayotoa bima ndogo, mteja anaweza kujiandikisha kupokea huduma hii kwa kupiga *148*15#.

Hitimisho

Kenya na Tanzania zina asilimia kubwa ya wananchi wa kipato cha chini. Idadi hii ya watu ambao hawazingatiwi mara nyingi huona sera ya bima kama anasa ama uraibu. Kwa bahati nzuri, kuna kampuni chipuzi mbalimbali za bima ya kisasa ambazo zimeweza kutumia teknolojia ya ubunifu na hivyo kuibua mabadiliko ya hali kama ilivyo. Taasisi zilizojadiliwa katika makala haya ni baadhi ya kampuni ambazo zimekuwa zikichangia kupunguza umaskini katika eneo hili kwa kuwatolea watu wenye kipato cha chini sera ya bima kwa gharama nafuu.