Mawazo ya Biashara Chipukizi Barani Afrika Mwaka 2022

Tafsiri:
amen_US

Afrika ni mojawapo ya maeneo yanayokua kwa kasi duniani. Iko katika awamu ambapo serikali na sekta binafsi zinajitahidi kuendeleza huduma zilizopo na mifumo ili kuambatana na zile za nchi zilizoendelea. Wawekezaji wa ndani mwa nchi na wa kimataifa Afrika wana nafasi nzuri ya kupata mapato makubwa kuliko katika maeneo mengine ya dunia. Hivyo basi, makala haya yatazungumzia baadhi ya mawazo ya biashara chipukizi katika Afrika kwa 2022.

startup ideas in Africa
Biashara chipukizi, Twiga Foods, inawaunganisha wakulima vijijini na wachuuzi wa mijini nchini Kenya.

Kwa Nini Uanzishe Biashara katika Afrika?

Rasilimali kutokana na idadi ya watu. Katika muongo uliopita, pameibuka taasisi nyingi nzuri za kielimu. Hii imesababisha kuwepo kwa idadi kubwa ya vijana wenye elimu ambao ni mojawapo ya rasilimali inayoathari mifumo ya ujasiriamali.
Uchapuzi wa kibiashara. Kwa biashara chipukizi, awamu ya kwanza ya kuendesha biashara inaweza kuwa yenye changamoto. Biashara chapuzi hivyo basi huafiki kutoa msaada kwa biashara ndogo na za wastani(SMEs) ili kukabiliana na vikwazo vinavyohusiana na miundombinu, viungo vya masoko, ufadhili, na ujuzi wa ujasiriamali.
Kuendelezwa kwa usasa na ukuaji wa miji. Idadi kubwa ya Waafrika inaendelea kuhamia katika miji iliyoendelea na inayoendelea ndani ya bara la Afrika. Zaidi ya hayo, miji hii ina sifa ya maendeleo na maisha ya kisasa. Mambo haya huweka msingi mzuri kwa ajili ya mawazo mbalimbali ya biashara chipukizi katika Afrika hasa mwaka wa 2022.

Vitovu vya Uvumbuzi / Vitovu vya Biashara Chipukizi

Je, ni Changamoto Zipi Zinazokumba Shughuli za Biashara Katika Afrika?

Miundombinu Duni. Licha ya kuwa na ubora wa hali ya barabara kuu mbalimbali katika nchi za Afrika, bado ni vigumu kutumia njia fulani. Zaidi ya hayo, kuna baadhi ya maeneo ambayo bado hayana umeme.
Misukosuko ya kisiasa. Katika baadhi ya nchi za Afrika, ni kawaida kuzuka kwa vita wakati wa mabadiliko ya utawala. Katika kipindi kama hicho, taifa hilo huathirika kiuchumi kwa kiasi kikubwa kwani wawekezaji na wateja hupunguza matumizi yao kwa hofu ya waandamanaji kuharibu mali zao.
Kiwango cha juu cha ushuru. Kampuni katika baadhi ya nchi za Afrika mara nyingi zilitaja kiwango cha juu cha ushuru kama mojawapo ya changamoto zinazokabili biashara katika Afrika.Kodi ya juu kwa mapato huathiri mafanikio ya biashara chipukizi mbalimbali barani Afrika.

Mawazo ya Biashara chipukizi barani Afrika

Uchukuzi wa Mjini

Kumekuwa na ongezeko la idadi ya maeneo ya mijini katika Afrika na idadi ya watu katika miji iliyopo kuongezeka kwa kasi. Umoja wa Mataifa una makadirio kwamba idadi ya watu mijini katika maeneo haya itaongezeka kutoka asilimia 11.3 mwaka 2010 hadi asilimia 20.2 mwaka 2050. Maeneo haya ya mijini yana majukumu muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika. Hii hasa ni kwa sababu maeneo haya hujenga mahitaji makubwa kwa ajili ya bidhaa mbalimbali na huduma, na kuhusisha kampuni za sekta mbalimbali, na kuzijumuisha nchi nyinginezo.

Ili kuibua ufanisi na kutimiza wajibu wa miji katika ukuaji wa uchumi, ni lazima kuwe na mtiririko huria wa bidhaa kutoka maeneo ya vijijini hadi miji ndani na nje ya nchi. Hii basi inafafanua jukumu la uchukuzi wa mijini. Hata hivyo, sekta hii imekuwa inakabiliwa na matatizo makubwa kama vile miundombinu duni na msongamano. Kama sekta nyingine yoyote, fursa bomba huibuka kutokana na changamoto kama hizi. Hivyo hii ni moja ya biashara ya kufanya 2022.

Washiriki wa sasa wanathibitisha kwamba uchukuzi wa mijini ni moja ya mawazo bora ya biashara chipukizi katika Afrika. Kwa mfano, kuna mahitaji makubwa ya mazao ya kilimo katika miji lakini wakulima wadogo wadogo katika maeneo ya vijijini mara nyingi wana ugumu wa kusafirisha mavuno yao sokoni kutokana na vikwazo vya miundombinu.

Biashara chipukizi kama Twiga Foods nchini Kenya imejitahidi kuziba pengo kwa kuunganisha wakulima vijijini na wachuuzi mijini. Hii ni biashara chipukizi yenye faida kwani mtu anaweza kutegemea uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo katika maeneo ya mijini kwa kuyapata kutoka mashambani kwa bei nafuu na ubora wa kuridhisha.

Uchukuzi wa Biashara-hadi-biashara (B2B) pamoja na matumizi ya kidijitali katika huduma zinazotolewa ni maeneo mojawapo ambayo unaweza kutumia ili kujinufaisha. Kwa mfano, unaweza kuamua kutoa huduma au biashara za usafiri kwa bei nafuu. Katika enzi hizi za biashara za kimtandao, mahitaji ya huduma kama hizi ni ya kiwango cha juu barani Afrika.

Makazi Nafuu

Makazi ya staha ni mojawapo ya mahitaji ya msingi ya binadamu. Hata hivyo, hii bado imesalia kuwa ndoto isiyotimia kwa idadi kubwa ya Waafrika kwenye maeneo ya vijijini na mijini. Katika maeneo ya vijijini, watu wengi wanaishi kutokana na mapato kidogo. Baadhi yao wanajitahidi kukidhi mahitaji ya chakula kwa wategemezi wao na hivyo hawawezi kujitwika tena mzigo wa mawazo ya kupata nyumba nzuri.

Tatizo kama hilo pia limethibitishwa katika maeneo ya mijini. Makazi duni mengi katika miji ya Afrika ni makazi ya watu maskini ambao hawana uwezo wa kukimu kodi ya nyumba bora. Vilevile, tabaka la kati halijasazwa. Wengi wa Wafrika katika tabaka la kati hawawezi kutimiza ndoto yao ya kumiliki nyumba katika mazingira tulivu. Hivi sasa, vipande vya ardhi na nyumba zilizoko ndani na karibu na miji ni ghali sana kutokana na ongezeko la mahitaji yake.

Kwa kuyafahamu maswala haya, mtu anaweza kuendeleza biashara yenye mafanikio kwa kutoa uvumbuzi wa makazi ya gharama nafuu katika nchi tofauti za Afrika. Mojawapo ya njia ya mawazo ya biashara chipukizi ni kupitia kwa ununuzi wa ardhi kutoka maeneo yaliyozingira miji na kugawanya na kuuza vipande vya kwa bei nafuu kwa wateja walengwa. Unaweza pia kuchagua kujenga nyumba za bei nafuu ili kuvutia tabaka la chini na kati la wakazi.

Kutoa bidhaa nafuu kwa watu binafsi na wahusika katika sekta ya mali isiyohamishika ni njia nyingine ya faida ya kuibua biashara chipukizi katika masoko yanayochipuka ya Afrika kama vile Kenya, Tanzania, Rwanda, na Ethiopia miongoni mwa nyingine. Hii inaweza kuwa kitu chochote ikiwemo vifaa vya ujenzi, samani na bidhaa nyingine za kuboresha nyumba.

Kilimo cha Kimakundi

Mtu anaweza kujiuliza, kama asilima 60 ya ardhi ya dunia inapatikana katika bara la Afrika, basi kwa nini pana sifa ya upungufu wa mara kwa mara wa chakula na wakulima maskini? Licha ya kuwa kuna sababu kadhaa za kimsingi, ukosefu wa rasilimali zinazohitajika katika awamu mbalimbali za kilimo ni mojawapo ya sababu za msingi. Wakulima wengi wadogo wadogo wanalazimika kutegemea mbinu za kilimo za kisasa; swala linalowafanya kuwa na uzalishaji mdogo.

Ujasiriamali wenye matokeo ni moja ya suluhuhisho la kuaminika kwa tatizo hili. Hii ni kanuni ya msingi kwa kilimo cha kimakundi. Umoja wa Mataifa unakadiria ya kwamba sekta ya kilimo cha biashara katika Afrika itakuwa na thamani ya dola trilioni 1 katika mwaka wa 2030.

Si lazima ujihusushe moja kwa moja na shughuli za kilimo hiki ili upate mgao wako wa faida. Kilimo cha kimakundi/umati ni mfumo wa biashara ya kilimo ambapo watu binafsi kutoka sehemu yoyote ya dunia wanaweza kuwekeza katika mradi mahususi wa kilimo na kupata sehemu yao ya mapato ya mkulima waliyekeza kwake.

Farmcrowdy ni mfano wa mfumo wa kilimo cha faida cha kimakundi/umati katika Afrika. Mfumo huu ulianzishwa nchini Nigeria mwaka 2017 kama biashara ya kwanza ya kilimo cha kisasa katika kanda ambayo inawaunganisha wawekezaji na wakulima. Mapato yanayozalishwa yanagawanywa baina ya wawekezaji, wakulima, na kampuni. Kwa njia ya mfumo huu, biashara hii imeweza kufikia zaidi ya wakulima wadogo wadogo milioni 38.

Farmcrowdy ni mfano mwafaka wa jinsi mtu anaweza kufanikiwa katika sekta pana ya kilimo bila ya kuhusika na shughuli za kilimo halisi. Zaidi ya hayo, huhitajiki kufanya kazi kama kampuni kubwa katika awamu za mwanzo. Unaweza kujiunga na kikundi cha rafiki zako au jamaa na kisha kuwatafuta wakulima wa kuwekeza katika shughuli zao za kilimo.

Siri ya faida ya kilimo hiki cha kimakundi ni kutambua mazao ya biashara yenye faida kubwa na mfumo wa kilimo wenye mapato ya juu na hatari ya chini ya hasara.

Mazao ya biashara yenye faida kubwa 2021 ni pamoja na mahindi, ngano, mtama, maharage, mihogo na mchele.

 

Huduma za Afya ya Kisasa

Afrika ina takriban asilimia 25 ya magonjwa yote duniani lakini zaidi ya nusu ya idadi ya watu hawana uwezo wa kupata huduma bora za matibabu au bima ya afya. Pamoja na utepetevu wa viongozi kuhusiana na hali ya huduma za afya, umaskini pia ni mojawapo ya sababu kuu za changamoto hizi.

Huku nchi nyingi za Afrika zikiwa katika kundi la mataifa ya ulimwengu wa tatu, kuna ukosefu wa fedha za kutosha ili kuanzisha hospitali za kutosha za kisasa kwa wananchi wake. Hii imesababisha Waafrika wengi kutembea mbali sana ili kutafuta huduma za msingi za afya na hata imekuwa kama hali ya kawaida katika vyombo vya habari.

Angazia hali hii: mwanamke mjamzito anapotambua baadhi ya mabadiliko kidogo katika hali ya mwili wake na hana uhakika kama ni jambo la kawaida kwa ujauzito au kama anapaswa kuwa na wasiwasi. Wazo la kutembea kwa kilomita 10 na kugharamia ada zote zinazohitajika kwa ajili kupokea mashauriano ya matibabu huwa kero. Kwa kuwa Waafrika wengi wanaweza kuwa na simu ya mkononi, haitakuwa afueni kwake akipata kujua kwamba anaweza kupokea majibu kwa maswali yake kwa faraja nyumbani mwake?

Wajasiriamali wanaweza kusaidia kutatua tatizo hili, na kuendeleza biashara yenye faida katika harakati hiyo, kwa kuanzisha nyenzo za kidijitali zinazounganisha umma na wataalamu mbalimbali wa matibabu. Kwa mfano, mfumo huo huweza kujumuisha njia za mawasiliano za wataalamu wenye vibali, huduma za dharura, na maduka ya dawa katika sehemu mbalimbali nchini. Agence Française de Developpement nchini Tunisia ni mfano mzuri wa mradi mwafaka unaosaidia katika kutoa huduma za afya za kisasa kwa njia ya simu.

 

Uratibu wa Sherehe na Matukio

Katika kipindi cha hivi karibuni, Waafrika wengi wameishia kupendelea usimamizi wa sherehe na matukio. Kinyume na kujihusisha na maandalizi yote wakati tukio maalum, watu wengi huamua kukodisha huduma za kitaalamu ili kuratibu kila kitu. Ili kupata faida miongoni mwa washindani wengine katika biashara hii, unahitajika kupanua mawanda yako ya kazi.

Licha ya kuwa ni muhimu kuteua walengwa mahsusi, huenda ukalazimika kuongeza makundi ya wateja wako kwa kutoa huduma zako katika mazishi, harusi, sherehe za siku ya kuzaliwa, matukio ya kimashirika, na vikao vinginevyo. Zaidi ya hayo, huenda ukawazia kutoa huduma pana na ya kina ili kuimarisha mafanikio yako katika wazo kama hili la biashara chipukizi.

Badala tu ya kutoa huduma ya mahema, viti, na kurembesha maeneo, unaweza kushirikisha pamoja na vitu vingine muhimu kama vinywaji na chakula, msimamizi, mitambo ya burudani, watumbuizaji, na hata huduma za usafiri.

Kwa kifupi, ni muhimu kujitahidi kuwa mtu anayetegemewa na aliyekamilika kwa ajili ya shughuli hii ya mipangilio ya sherehe na matukio katika eneo lako. Uratibu na usimamizi wa sherehe na matukio unazidi kupokelewa vyema Afrika.

Hitimisho Kuhusu Mawazo ya Biashara 2022

Afrika inazidi kukua na kupevuka. Hivyo basi, huu ni wakati bora wa kutambua na kutekeleza mojawapo ya biashara za kufanya 2021. Ingawa kuna changamoto nyingi wanazokabiliwa nazo wajasiriamali katika miaka yao ya kwanza ya kibiashara, bara hili limejaa fursa za faida kubwa za kibiashara. Kwa uvumilivu na mipangilio ya mikakati ya ufanisi, pana uwezekano wa kuwa mmoja wa wafanyabiashara wenye mafanikio katika bara la Afrika.