Nguzo za Mafanikio ya Ujasiriamali Afrika

Tafsiri:
No available translations found

Kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira wanachokabiliana nacho vijana kimeendelea kuibua wasiwasi kubwa duniani kote. Kimataifa, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana ni suala linalotia wasiwasi kwani kilikuwa asilimia 13.1 katika mwaka wa 2017. Kiwango hiki cha ukosefu wa ajira kimesababisha vijana kutegemea ubunifu wa biashara kupata kipato. Makala hii itakuonyesha jinsi ya kufanikiwa katika biashara kama mjarisiamali.

**Ujarisiamali ni nini?** Ujasiriamali ni uwezo na nia ya kuendeleza, kuandaa na kusimamia mradi wa kibiashara pamoja na uwezekano wowote wa hatari ya hasara ili kupata faida. — BusinessDictionary

Vikwazo vya Ujasiriamali Afrika

  • Ukosefu wa elimu ya ujasiriamali na ujuzi.
  • Ukosefu wa tajriba ya awali ya ujasiriamali au uzoefu wa kazi.
  • Ugumu wa upatikanaji wa taarifa au ufadhili.
  • Changamoto ya masoko au kukosekana kwa masoko na mitandao, na mazingira dhaifu ya kutoa usaidizi kwa ujasiriamali.

Nguzo za Mafanikio ya Ujasiriamali

Ujasiriamali si rahisi. Kulingana na Faharasa ya Aprili 2014 ya Kauffman ya Shughuli za ujasiriamali, asilimia 0.28 ya watu wazima kila mwezi walianzisha biashara mpya mwaka 2013. Kati ya wafanyabiashara hawa wapya, wengi hawakufanikiwa kuendelea. Hivyo basi, ni nini hutenganisha biashara yenye mafanikio mbali na ile iliyofeli? Na ni zana zipi ambazo mjasiriamali chipuzi anahitaji ili kufanikiwa?

Makala haya yataangazia baadhi ya nguzo zinazotambulisha mafanikio ya ujasiriamali wowote.

Aina za ujasiriamali. Ujasiriamali uko wa aina nyingi. Lakini aina zote zinaangukia kwenye makundi makubwa matatu: ujasiriamali kulingana na mjasiriamali, ujasiriamali kulingana na saizi na ujasiriamali kulingana na ubunifu.

1. Wazo na Soko

Wazo linahusu aina ya biashara unayotaka kufanya huku soko ni watu ambao watanunua bidhaa au huduma yako. Wazo zuri ni msingi wa mradi wenye mafanikio. Upatikanaji wa soko huashiria uendelevu wa mradi wa kibiashara. Unahitaji kutenga muda wa kutosha ili kutafiti wazo la biashara, soko na kutathmini mahitaji ya bidhaa au huduma yako. Mafanikio ya biashara chipuzi na kustawi kwake hutegemea uwezo wa “kuongeza thamani kutokana na tatizo.”

Mwaka 2010, Lorna Rutto (Kenya) aliacha kazi yake ya benki na kuanzisha biashara ya kusaga taka, ili kujaribu kutatua tatizo hilo. Kampuni yake, EcoPost, hukusanya na kufanya upya tena plastiki kwa kutengeneza mihimili ya kujengea nyua (uzio) yenye kupendeza na kudumu muda mrefu na pia salama kwa mazingira, kama nyenzo mbadala kwa mbao.

how to become an entrepreneur
Lorna Rutto, mjasiriamali mwanzilishi wa EcoPost.

Mikopo ya ujasiriamali. Ikiwa unataka mikopo ili kuwezesha wazo lako la ujasiriamali kuwa la kweli, tazama hapa mikopo binafsi kwa simu. Unaweza pia kutumia huduma kama za Venture Capital for Africa ambazo zinawasaidia wajasiriamali kupata mitaji bila kuomba mikopo.

2. Kuchambua na Kufahamu Washindani Wako

Ili biashara yako iwe na mafanikio, unahitaji kuelewa wale unaoshindana nao. Unahitajika kuweka rekodi kuhusu washindani wako na kubainisha kile wanachofanya kwa njia mwafaka au jinsi gani unaweza kulinganishwa dhidi yao. Tafiti washindani wako vizuri ili kujua uwezo na udhaifu wao. Pia, tathmini aina ya tishio kutokana na washindani wako kwa biashara yako. Kwa kuchambua washindani wako, pana uwezekano wa kujua jinsi ya kutumia udhaifu wao ili kuimarisha biashara yako.

3. Jitihada

Hii ni nguzo nyingine muhimu ambayo huhakikisha mafanikio. Unahitaji kufanya kazi kila siku na kutoa huduma na bidhaa zenye ubora. Kuna haja ya kuishughulikia biashara kama mradi maalum na wala si shughulu mbadala. Kwa kuchukulia mradi wako wa ujasiriamali kwa uzito utawafanya watu kukutegemea pia.

entrepreneurship guide
Anna Phosa, ‘mkulima maarufu wa nguruwe’ Afrika Kusini.

Anna Phosa ni mmoja wa wakulima wa Afrika wenye mafanikio ya ufugaji wa nguruwe. Yeye mara nyingi hujulikana kama ‘mkulima maarufu wa nguruwe’. Hata hivyo safari yake ya biashara haikuwa rahisi kwani alipata ugumu wa kupata mtaji wa kuanzisha na kukuza biashara.

Mwaka 2004, Anna alianzisha ufugaji wake wa kwanza wa nguruwe katika shamba la Soweto akitumia dola 100 kutoka kwa akiba yake binafsi. Alianza akiwa na nguruwe wadogo wanne tu. Baada ya miaka minne – katika mwaka wa 2008 – alipokea mkataba wa Pick ‘n Pay wa kusambazia maduka yao nguruwe 10 kwa wiki. Haya yalikuwa ni mafanikio ya kwanza na ombi hili lilikua haraka hadi usambazaji wa nguruwe 20 kwa wiki.

Kufikia mwaka wa 2010, alisaini mkataba mkubwa na Pick ‘n Pay wa kusambaza nguruwe 100 (kwa wiki) kwa zaidi ya miaka mitano iliyofuata kwa kima cha Randi milioni 25 – hiyo ni karibu dola milioni 1.9. Hii yote ilitokea kwa sababu ya bidi yake ya kazi na kujituma.

4. Usimamizi wa Rasilimali na Utulivu wa Kifedha

Wajasiriamali wengi hutambua mtaji wa fedha kama changamoto yao kubwa wakati wowote wanapojaribu kuzindua mradi wao wa ujasiriamali. Usimamizi wa rasilimali unahitaji utunzaji sahihi wa kumbukumbu na hati za kila kitu kuhusu fedha ndani ya biashara. Hii huhakikisha nidhamu ya kifedha na matumizi kwa njia ya busara ya rasilimali zilizopo.

Kuna njia nyingi kwa njia ambazo unaweza kutumia ili kuzalisha mtaji wa awali, ikiwa ni pamoja na akiba ya binafsi, mikopo, misaada au michango kutoka kwa marafiki na familia.

Licha ya kutoka katika historia ya umaskini katika vitongoji vya Addis Ababa, Bethlehemu Alemu aliweza kupata michango kutoka kwa familia na jamaa yake. Ndoto yake ya biashara haingeweza kunawiri bila ya mtaji wa dola 10,000 kutoka kwa familia na jamaa mwaka wa 2004. Biashara yake – SoleRebels – ni moja ya zile maarufu na bidhaa za viatu zinazokuwa kwa kasi katika dunia! Mkusanyiko wake wa viatu vilivyo salama kwa mazingira (huvitengeneza kutokana na vifaa vilivyotengenezwa upya) huuuzwa katika nchi zaidi ya 50 duniani kote, ikiwa ni pamoja na Marekani, Canada, Japan na Uswisi. Msukumo wake wa mafanikio umeangaziwa kwenye Forbes, BBC na CNN. Alielezwa na Forbes kama ‘Mmoja wa Wanawake Shupavu sana Duniani’

entrepreneurship tips
Bethlehem Alemu, mwanzilishi wa kampuni ya SoleRebels.

5. Zingatia Mahitaji ya Wateja Wako

Ili biashara yoyote iwe na mafanikio, wateja lazima wahusishwe katika shughuli za biashara na malengo ya kila siku. Maoni mazuri na mabaya yanahitaji ya kuzingatiwa. Mjasiriamali anahitaji kujumuisha pongezi na malalamiko yote ili kutoa huduma bomba kwa wateja.

Wakati mwingine, biashara huanzishwa kutokana na mahitaji, matatizo au malalamishi haya kutoka kwa wateja katika soko lako. Dominic Mensah, Prince Boakye Boampong na Jesse Arhin Ghansah walianzisha OMG Ghana mwaka 2012 wakati walikuwa chuoni. Simu za kisasa ndio mwanzo zilikuwa zinaanza kuwa maarufu zaidi wakati huo. Hivyo, waliamua kuanzisha kampuni ya huduma za habari ambayo ingetoa huduma hiyo kwa vijana Waafrika wanye ujuvi wa kimtandao. Leo, nembo na huduma za kampuni hii zimeweza kuenea kutoka Ghana hadi Nigeria na Kenya. Pia, inalenga kufanya uzinduzi huko Afrika Kusini, Uganda, Zambia na Tanzania.

how to become an entrepreneur in Africa
Dominic Mensah, Prince Boakye Boampong and Jesse Arhin Ghansah, waanzilishi wa OMG Ghana.

6. Uwezo wa Kujifunza Mara kwa Mara

Mafanikio ya wajasiriamali hutegemea kujifunza tena na tena kwa njia mpya za kutatua matatizo au njia mpya za kuboresha shughuli zilizopo. Wanapaswa kuwa macho na daima kuwa na hamu ya maarifa mapya, ujuzi na mwelekeo wa fikira ambao unawawezesha. Wanahitajika kujifunza kutoka kwa wengine, hasa wale ambao tayari wamefanya mambo sawia ya ujasiriamali. Wajasiriamali wanaweza kupitia mzunguko mzima wa ujasiriamali na kufanikiwa. Lakini, ili wawe na mafanikio ya kudumu, pana haja ya kuendelea kukua bila kutekwa katika mitego ya kuhisi kuwa na faraja na kuridhika.

Hali Ya Ujasiriamali Barani Afrika

Afrika inazidi kuchukua nafasi yake katika jukwa la kimataifa kama bara lenye kukuza uchumi na fursa. Ujasiriamali barani Afrika ni muhimu katika ustawi wa baadaye wa Afrika. Wajasiriamali wa Afrika pia wanaonekana kuwa wanaendelea kupitia mabadiliko. Kwa kawaida, wajasiriamali wamekuwa wanaume. Pengo la kijinsia linazidi kutoweka katika nchi za Afrika kama Angola, Botswana, Nigeria, Afrika Kusini na Zambia.

Linapokuja suala la wanawake kumiliki biashara, nchi mbili za Afrika zipo juu ya orodha duniani kote. Uganda iko kileleni na asilimia 34.8 ya biashara zinazomilikiwa na wanawake, huku Botswana ina asilimia 34.6. Kiwango hiki cha umiliki ni cha juu zaidi kuliko mataifa kama Marekani, Uingereza na Ujerumani.

Matokeo ya faharasa hii yalibaini kuwa wajasiriamali wa kike katika nchi zinazoendelea walionyesha ushujaa, kujiamini na kuwa na hamu ya kuzisaidia familia na jamii zao. Hii inaonyesha kwamba wajasiriamali wanawake ni uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi na maendeleo, hasa katika bara la Afrika.

Hitimisho

Katika nyakati hizi ambapo kuwa mjasiriamali imekuwa rahisi, nguzo hizi za kimawazo za ujasiriamali ni muhimu hata zaidi. Kama unataka kuanzisha biashara inayostawi katika karne ya ishirini na moja, utahitajika kuwa na mabadiliko ya kidhana. Huwezi tu kurudufu kinachoendelezwa katika soko na kisha utarajie kutawala. Unatakiwa kuelewa kuwa inahitaji zaidi ya mawazo mazuri ili kuwe na mafanikio katika biashara. Itakugharimu mipango sahihi, mikakati, malengo, mifumo bora na shughuli zinaozingatia wateja ili kufanikiwa katika biashara ya leo.