Mawazo ya Kibiashara Kwa Wanafunzi Vyuoni

Kama mwanafunzi, unaweza kuwa na muda mwingi wa kujihusisha na shughuli za ujasiriamali. Kuna fursa mbalimbali za kibiashara ambazo wanafunzi wa vyuoni wanaweza kuanzisha bila gharama kubwa ya mwanzoni au kuhitaji kutenga muda mwingi sana. Maelfu ya wanafunzi wanajichumia mapato kupitia biashara ndogo zenye faida kubwa. Haya hapa ni baadhi ya mawazo ya biashara nzuri kwa wanafunzi.

Kufungua Mgahawabwaka (Cyber Café)

Kwa kuwa tumo katika dunia ya kidijitali, watu wengi wanna kiu ya kupata habari mpya. Katika vyuo, wahadhiri na wanafunzi wanafanya utafiti zaidi na ili kuwezesha hili, ni lazima kuwa na mfumo bora wa mtandao. Huenda isiwe rahisi kwa kila mtu kutumia mtandao wa Wi-Fi unaopatikana chuoni. Kwa sababu hiyo, kwa kuanzisha mgahawabwaka, itakuwa fursa muhimu na chanzo cha maarifa kwa wale ambao wanataka kujua zaidi. Mgahawabwaka ni fursa ya kibiashara thabiti na yenye faida sana.

Duka la Kurudufisha

Katika mazingira ya ufunzaji, huduma za kupiga chapa ni muhimu na za lazima. Kuanzisha biashara ya kurudufisha kama mwanafunzi ni wazo zuri. Isitoshe, unaweza hata kuzungumza na wahadhiri wako wawe wakiwacha makala ya kazi katika duka lako ili wanafunzi wayachukue kwa gharama ndogo. Unaweza pia kuuza vifaa vinginevyo kama kalamu na vitabu katika duka lako.

Uandishi wa Habari za Mtandaoni (Kublogu)

Uandishi wa habari mtandaoni, kublogu, ni mojawapo ya njia rahisi na ya haraka ya kujipatia fedha. Kama una ari ya kuandika habari, hadithi za kidhahania, siasa, na hata habari za uvumi, unaweza kuunda blogu na kuwaelekeza wasomaji kwenye wavuti wako, na kisha unaweza kuanza kupokea mapato kutoka Google, au hata kampuni ambazo zingependa kufanya matangazo kwenye wavuti wako. Hakikisha kuwa umejisajili kama mwanachama wa Bloggers Association of Kenya (BAKE).

Duka la Kuuza Mavazi

Wanafunzi wa vyuoni wanapenda kuvalia nadhifu kwa mtindo wa kisasa. Biashara hii itakuwa na soko la tayari wakati wowote. Kama mwanafunzi, unahitaji tu kufanya utafiti wa mavazi yanayovuma kimtindo na upo tayari kwa biashara hii. Unahitaji kuwa na duka lililopo katika eneo la kimkakati na kupata fedha za kutosha ili uweze kuwa na aina tofauti ya nguo na bidhaa za mitindo kutoka kwa wanamitindo mbalimbali. Iwapo duka halipatikani, unaweza kuuza vitu yako katika eneo wazi, hasa nyakati za jioni. Kwa kufanya hivi utajihakikishia mtiririko wa mapato.

Kufungua Kituo cha Biliadi

business ideas kenyan students

Kama una makini ya kufanya biashara chuoni, utagundua kuwa mchezo ya biliadi ni yenye mnato sana. Hii ni kwa sababu pindi unapoanza kucheza utalazimika kurejea tena na tena kutokana na uraibu huo. Kama mjasiriamali unahitajika kuchukua nafasi hii na kuigeuza kuwa chanzo cha mapato. Unaweza pia kuamua kuuza vinywaji katika kituo hiki cha biliadi ili kuwanasa wateja wako hata zaidi.

Michezo ya Video

Michezo ya video ni maarufu kama mojawapo ya njia za kujiburudisha nchini Kenya. Wanafunzi wa vyuoni wanaweza kufurahia kucheza michezo ya video wakati wa muda wao wa mapumziko na hata mwishoni mwa wiki. Unahitajika tu kuwa na eneo la kimkakati na upo tayari kuendelea na biashara hii.

Kuuza Maua na Kadi za Misimu Zilizobinafsishwa

Kama mwanafunzi wa chuoni, hii ni mojawapo ya fursa bora ya biashara unayoweza kuijaribu. Kuadhimisha siku za kuzaliwa katika chuo kikuu ni kama utamaduni. Hii ina maana kwamba wakati wowote ule, kutakuwa na soko la tayari kwa kadi zilizobinafsishwa za salamu. Msimu kama wa Wapendanao (Valentines), kadi na maua daima huwa na uhitaji mkubwa. Kuifanya biashara hii kwa wakati kama huu itakuwa na mapato mazuri.

Kukarabati Kompyuta na Simu za Mkononi

Karibu kila mwanafunzi katika chuo kikuu anamiliki simu. Vifaa hivi ni muhimu kwa ajili ya masomo, na huwa kero endapo vitaharibika. Wanafunzi wenye mawazo ya kibiashara watajibidiisha kupata ujuzi wa kiufundi wa jinsi ya kutengeneza simu na vipakatalishi. Ajira ambazo zinahitaji ujuzi wa kiufundi hulipa vyema, kwa kuwa watu wengi hawajishughulishi nazo na hivyo kuwa wazo bora la kibiashara.

Kuuza Muziki na Video

Wanafunzi wengi wanayapendelea mambo ya muziki. Kuwa muuzaji wa rejareja wa muziki na video ni mojawapo ya biashara yenye faida kubwa ambayo wanafunzi chuoni wanapaswa kuijaribu. Wanafunzi pia hutazama sinema na kusikiliza muziki wakati wa muda wao wa mapumziko. Biashara hii ni ya ushindani sana, na ili uwahifadhi wako, ni lazima ufanye utafiti wa kina na kujua kuhusu muziki mpya na sinema na filamu maarufi katika kipindi kilichopo.

Kupiga Picha

Kama unapenda kupiga picha, hii ni nafasi yako ya kupata pesa kutokana na shughuli hii. Unahitaji tu kamera, mwanga, vifaa vya kudhibiti mwanga na ujuzi wa kupiga picha. Unaweza kutumia wikendi na kupiga picha katika harusi, mikutano, na sherehe mbalimbali. Unaweza pia kutoa huduma ya kupiga picha na kuziuza kwa familia na watu binafsi. Unaweza pia kuuza picha zako kwenye soko la mtandao kama vile AfricanStockPhoto.

Kuanzisha Biashara ya Kuuza Vyakula

business ideas kenyan students

Kwa kawaida kuna mengi ya kufanya chuoni. Kutokana na shughuli nyingi zinazoendelea, wanafunzi wengi hawapati nafasi ya kupika wanamokaaa. Hii ni nafasi ya kipekee ya kuanzisha biashara. Biashara hii itakuwa na soko la tayari wakati wowote. Unaweza hata kujaribu kuandaa vyakula maalumu; vile ambavyo havipatikani katika sehemu hiyo ya nchi.

Kama una ujuvi wa kuoka, unaweza kutengeneza keki katika hoteli yako. Unaweza pia kuuza keki hizi kwa kutembelea maeneo ya makazi mbalimbali chuoni wakati una muda. Unaweza pia kuoka kwa shughuli na sherehe kama harusi, siku za kuzaliwa na maadhimisho ya kipekee ili kupanua soko lako. Hii inaweza kuwa shughuli yenye faida sana kwako.

Biashara ya Ususi

Biashara zinazowalenga wanawake hustawi vizuri. Duka la ususi ni biashara ya faida kubwa sana ambayo mwanafunzi wa kike anaweza kuanzisha. Ni biashara inayohitaji muda mwingi, na inakuhitaji kusawazisha kati ya masomo na biashara. Ili kuwa na wateja wengi, unahitaji kujua mitindo ya nywele inayovuma. Kwa kuweka akiba ya mitindo ya nywele na bidhaa za nywele, utajihakikishia idadi kubwa ya wateja. Unaweza pia kwenda kwenye maeneo wanamokaa wateja wako ili kuziuza bidhaa zako.

Kutoa Huduma za Dobi

Baadhi ya wanafunzi ya chuoni hupenda kuonekana nadhifu lakini hawana subira au muda wa kutosha wa kujifanyia shughuli za kufua wao wenyewe mara kwa mara. Unaweza kuanzisha biashara ya kufua ambapo utakuwa unatoza ada ndogo. Huhitaji kuwa na mtaji mkubwa au ujuzi wa kipekee kwa kazi hii; unahitaji tu muda wako.

Biashara ya M-Pesa

mpesa
M-Pesa ni huduma ya fedha kwa njia ya simu inayoongoza nchini Kenya.

Biashara ya M-Pesa ni yenye ushindani sana. Kama chuo unamosomea kuna idadi kubwa ya wanafunzi, kutakuwa na soko la tayari na biashara yako ina uwezo wa kustawi vizuri. Unaweza hata kuchukua fursa hiyo ya kibiashara kwa kuuza kadi za mjazo wa maongezi. Hebu fikiria kupokea mapato ya kila mwezi kutoka kwa mojawapo ya kampuni za mawasiliano nchini Kenya yenye faida sana; hili ni jambo la kutia moyo.

Biashara ya Kinyozi

Kila mwanafunzi wa kiume katika chuo kikuu anapenda kuonekana nadhifu. Baadhi ya wanafunzi wa kike wanapendelea kuweka nywele zao zikiwa fupi. Kama wewe ni mjuzi wa kunyoa na mapambo ya nywele, unaweza kutumia muda wa jioni na wikendi yako ili kujichumia fedha. Unaweza kupata eneo la kimkakati kwa ajili ya biashara, au ikiwa tu ndio unaanza, unaweza kuanza kwa kuwatembelea wateja katika nyumba zao au katika maeneo mliyokubaliana.

Ufanyakazi Huria wa Uandishi

Kama mwanafunzi chuoni, unaweza kupata pesa kwa njia ya uandishi. Kama una ari ya kuandika, basi unahitaji kujua mitandao bora ya kazi ya uandishi na kisha uanze kuandika. Baadhi ya tovuti unazoweza kutumia ili kujipatia riziki mtandaoni ni:

  • Fiverr. Unaweza kufanya kazi huria kwa ada inayoanzia dola 5. Unaweza kuandika makala au kujirekodi ukisoma shairi la mtu kwa sauti nzuri.
  • Upwork. Tovuti hii kwa sasa ndio bora na yenye wataalamu huria zaidi na ina pia ina kazi na wateja weledi. Waandishi hupokea mapato kutoka dola 5 kwa kila maneno 500 hadi dola 100.
  • Freelancer. Unaweza kupata kwa urahisi kazi yako ya kwanza katika tovuti hii. Malipo ya wastani ni dola 2 kwa kila maneno 500.
  • Homework Market. Tovuti hii inawaunganisha wanafunzi na wakufunzi ambao wanaweza kuwasaidia kufanya kazi zao. Unaweza kujibu maswali kulingana na taaluma yako.

Unaweza pia kutumia wavuti za ufanyakazi huria ya Afrika kama vile Kuhustle, Onesha, n.k. Tazama orodha ya wavuti hizi hapa.